Majaliwa awaelekeza ma-DC, RC vitambulisho wamachinga

26Apr 2019
Godfrey Mushi
DODOMA
Nipashe
Majaliwa awaelekeza ma-DC, RC vitambulisho wamachinga

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameagiza wakuu wote wa mikoa na wilaya nchini kutotumia nguvu au kulazimisha au kuwapa wajasiriamali wakubwa wenye mapato ya zaidi ya Sh. milioni 4 vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo,-

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa.

kwa sababu hali hiyo inaondoa maana ya uwapo wa vitambulisho hivyo vilivyotolewa na Rais John Magufuli.

“Sasa vitambulisho vile vilivyotolewa kwa wakuu wa wilaya, natambua kwamba maeneo mengine utekelezaji wake sio mzuri kwa sababu wako wengine wanalazimisha watu, badala ya kuwaelimisha namna ya kupata vitambulisho hivyo,” alisema Majaliwa.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga, wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.

Akitoa maelezo kuhusu vitambulisho hivyo, Waziri Mkuu alisema yapo maeneo wapo hata wajasirimali wakubwa wenye pato la zaidi ya Sh. milioni 4 ambalo linawafanya na wao washindwe kuchangia pato la taifa kulingana na biashara wanazofanya, kwa sababu wao kwa kipengele chao wanachangia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) moja kwa moja.

“Kwa hiyo waheshimiwa wabunge ni kwamba waheshimiwa wakuu wa wilaya na mikoa, (naelekeza) watumie muda wao kuelimisha, nani anapaswa kuwa na kitambulisho badala ya kutumia wakati mwingine nguvu au kwenda kulazimisha au kuwapa wajasiriamali wakubwa wenye mapato ya zaidi ya Sh.milioni 4 na kuondoa maana ya uwapo wa vitambulisho,” alieleza Waziri Mkuu.

Alisema serikali imeipokea hoja hiyo na wanaendelea kutoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, kutumia nafasi hiyo kuelimisha zaidi kuliko kulazimisha.

Waziri Mkuu aliwaasa wakuu wa mikoa na wilaya watumie nafasi hiyo kuelimisha ni nani anatakiwa apate kitambulisho hicho ili kuwaondolea usumbufu wa kuwa wanatozwa tena Sh. 200 au Sh. 500 kila siku mjasiriamali anapoendelea kufanya kazi yake ya kuuza mchicha, maandazi na wale wanaouza mahindi kwenye mabasi, kwa kuwa hao ndio ambao Rais Magufuli aliwalenga ili na wao waone uchangiaji wa uchumi, pato la nchi ni sehemu yao.

Aidha, alieleza kuwa nia ya serikali ni kuona pia wanaendelea kufanya biashara yao bila kusumbuliwa ndani ya mwaka kwenye halmashauri zao na kwamba serikali imeipokea taarifa hiyo na itaifanyia kazi zaidi ili kuleta utendaji ulio sahihi na wajasirimali waweze kujitoa kuchangia uchumi wao.

Akitoa ufafanuzi zaidi, Waziri Mkuu alisema ni kweli kwamba serikali imeweka utaratibu mzuri sana wa kuwafanya wajasiriamali wadogo waweze kuchangia pato la taifa na Rais Magufuli alibuni njia nzuri sana, ambayo inawatambulisha wajasiriamali hao.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, wajasiriamali hao wamewekwa kwenye madaraja yao, ambapo wapo wadogo, wamo wafanyabiashara wa kati na wajasirimali wakubwa.

Katika swali lake la msingi, Haonga alisema suala la vitambulisho kwa wajasiriamali wadogo wadogo limekuwa ni kero kubwa sana katika maeneo mbalimbali nchini na limekuwa ni kero kubwa kwa wale wajasiriamali wanaouza mboga kama michicha na nyanya, lakini hata wanaouza njegere, maandazi na vitumbua.

Alieleza  kibaya zaidi, maeneo mengine hata wale wanaotoka shambani amechuma mchicha wake anaambiwa naye ni mjasiriamali alipe Sh. 20,000 ili apewe kitambulisho.

USUMBUFU DHIDI YA WAWEKEZAJI

Kuhusu suala la wawekezaji wengi kudaiwa kukwamishwa na kusumbuliwa sana, Waziri Mkuu alisema ili kusimamia uwekezaji kwa ukaribu zaidi, Rais Magufuli aliunda Wizara mpya ya kushguhulika uwekezaji ili kusaidiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

“lengo hapa ni kuhakikisha kwamba tunaondoa usumbufu ambao wanaupata wawekezaji hao ili kuweza kuwekeza kwa urahisi zaidi. Hata hivyo kwenye uwekezaji sasa, tumefikia hatua nzuri sana, moja; tumetengeneza andiko maalum (Blue Print) ambayo imeonyesha njia rahisi za uwekezaji hapa nchini kwa lengo la kuondoa usumbufu kwa wawekezaji wetu na kwa hiyo tumetengeneza mazingira rahisi juu ya uwekezaji,” alieleza Waziri Mkuu

“Lakini mbili; tumeboresha kituo cha uwekezaji kwa kukaribisha wizara zote zinazoguswa na uwekezaji kwa kuwa na mtu wao pale kwenye taasisi ili mwekezaji anapokuja huduma zote kama alitakiwa kwenda wizara ya ardhi, akitaka kwenda Brela (Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni), tuna idara kama 10 au 11 ambazo ziko pale za kumhudumia mwekezaji na baada ya Wizara hiyo kuwa imeletwa Ofisi ya Waziri Mkuu.”

Habari Kubwa