Majaliwa awapa somo wapigakura

25Sep 2020
Neema Emmanuel
Misungwi
Nipashe
Majaliwa awapa somo wapigakura

WANANCHI wa Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza wametakiwa kufanya uamuzi sahihi na kumpigia kura kiongozi, atakayewaletea maendeleo bila kujali tofauti za vyama.

Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi wa Kata ya Misungwi, wilayani Misungwi, mkoani Mwanza, katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu jana. PICHA: OWM

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa, alitoa somo hilo wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Misungwi katika kampeni za uchaguzi.

Majaliwa alikuwa Misungwi kumwombea kura mgombea wa urais wa CCM, Dk. John Magufuli na wagombea ubunge na udiwani wa chama hicho.

Alisema, maendeleo hayana chama hivyo ni vyema wakamchagua kiongozi atakayeweza kuchapa kazi na kuleta maendeleo kwa Watanzania wote wakiwamo wanyonge.

Alisema wametekeleza miradi mbalimbali ikiwamo, maji na sasa wanateknolojia mpya ya kutoa maji ziwani, kwenda kwa wananchi.

Aliwataka wananchi hao kuwapeleka shule watoto kwa kuwa sekta hiyo imeboreshwa kwa kiwango kikubwa, pia mchakato wa kujenga mabweni kwenye shule za sekondari unaendelea.

Aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Charles Kitwanga, akizungumza na wananchi hao alisema serikali imefanya mambo mengi ikiwamo ujenzi wa hospitali mpya.

"Fedha za mradi huo wa maji Usagara, zimetoka mdogo wangu (Mnyeti) zisimamie hizo fedha zisije zikaenda kusikojulikana, usimamie vyema usije ukafanya mambo yetu yale mengine, kwa sababu CCM inasimamia maadili," alisema Kitwanga.

Naye mgombea wa ubunge wa Jimbo la Misungwi kupitia CCM, Alexander Mnyeti, alisema anachosubiri sasa ni kuwafanyia kazi wananchi hao.

Habari Kubwa