Majaliwa: Msichague kiongozi kwa upepo

12Sep 2020
Hamida Kamchalla
Tanga
Nipashe
Majaliwa: Msichague kiongozi kwa upepo

WANANCHI wa Jiji la Tanga wametakiwa wasirudie kosa walilofanya miaka mitano iliyopita kwa kufuata upepo na kuchagua kiongozi wa upinzani katika uchaguzi mkuu, badala yake wachague kiongozi wa mfano anayetekeleza ilani ya chama chake.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Ubunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa ametoa wito huo leo wakati akizindua kampeni ya CCM katika jimbo la Tanga uliofanyika katika viwanja vya Tangamano jijini hapa.

Majaliwa amesema kuwa katika jimbo hilo tayari yupo kiongozi anayefaa kupewa kura zote za ndiyo kutokana na kufanya utekelezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo Afya ambaye ni Ummy Mwalimu ambaye amefanya kazi nzuri katika wizara ya afya.

"Msichague kiongozi kwa upepo, tulia piga kura yako kwa utulivu, kuna mtu ameonyesha mfano katika uongozi wake akiwa Waziri wa Afya, mchagueni Dkt. Magufuli, mchagueni Ummy pamoja na madiwani wa CCM ili aendelee kuwasimamia katika maendeleo yenu" amesema Majaliwa.

Ameeleza kwamba serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji katika vituo vya Afya, Zahanati pamoja na hospitali ya wilaya ya Tanga ambapo kwa upande wa vituo vya Afya imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 3.3 kwa ajili ya ukarabati wa vituo vya Ngamiani, Duga na Mikanjuni na kurudi katika hali yake ya kawaida.

Aidha amesema kuwa shilingi Milioni 841 zimeletwa kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati mpya ya Kibafuta pamoja na kukarabati Zahanati tano za Kiruku, Kivuleni, Nguvumali, Mabokweni na Kwanjeka.

Habari Kubwa