Majaliwa, Zitto wamlilia Ruge Mutahaba

27Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Majaliwa, Zitto wamlilia Ruge Mutahaba

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza kwa niaba ya Rais John Magufuli amesema msiba  wa Ruge Mutahaba ni mkubwa kwa watanzania na serikali kwa sababu ametoa mchango mkubwa serikalini kwa kutafsiri fursa za viongozi wa nchi kuanzia awamu ya nne na ya tano.

Majaliwa amesema  Ruge alikuwa tayari kuwaongoza vijana kuwasaidia hata kwa kutumia fedha binafsi kuwafikisha kwenye matarajio yao.

"Jambo hili kwa serikali lilikuwa ni kubwa na ndio maana serikali imeendelea kushirikiana naye hata kwenye hili kwa sababu alisaidia vijana wetu kutambua umuhimu wa wao kuwa watanzania, umuhimu wa fursa tulizonazo kuzitumia vizuri na kwa wale walioshindwa kabisa kuwapa mwelekeo na wakati mwingine kuwashika mkono kuwapeleka mahali ambako panaweza kuwasaidia,"

Majaliwa amesema Ruge amewatumikia watanzania kwa kuzunguka nchi nzima kukutana na makundi mbalimbali ya watanzania kuwaeleza umuhimu wa kuitambua nchi  yao hasa uzalendo na kutambua fursa zilizopo.

Majaliwa amesema Ruge alibeba dhamana ya kuelimisha umma, kuhamasisha watanzania   na kushiriki kwa vitendo kuwahamasisha vijana kutambua na kutumia fursa mbalimbali ndani ya nchi.

Nae Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, amesema Ruge Mutahaba alikuwa kijana mbunifu ambaye ameshiriki kwa kiasi kikubwa kukuza vijana  wenzake na kuwa kiunganishi.

"Neno langu ni fupi sana kwamba tumepotelewa na Ruge lazima tusikitike,  lazima tulie lakini pia lazima tusherehekee maisha yake.

Ruge ameishi maisha ambayo ameacha alama," amesema Zitto.

Habari Kubwa