Majambazi yauawa, yakutwa na bunduki ya masista

16Mar 2016
John Ngunge
Nipashe
Majambazi yauawa, yakutwa na bunduki ya masista

BUNDUKI aina ya shotgun iliyoporwa katika Kituo cha Afya cha Nkoaranga, kinachomilikiwa na masista, imepatikana baada ya polisi kuua watu wawili walioshukiwa kuwa majambazi, usiku wa kumkia jana.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema ofisini kwake jana kuwa bunduki hiyo iliporwa katika kituo cha afya cha Tumaini, Februari 25, mwaka huu.

Alisema katika tukio la mauaji hayo, polisi walipata taarifa kutoka kwa msiri wao kwamba kuna majambazi ambao walipanga kuvamia Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha AVRCD kwa lengo la kuiba.

Kituo hicho kiko Kata ya Seela-Sing’isi, wilaya ya Arumeru.

Alisema majira ya saa tano za usiku, walijitokeza watu wanne waliokuwa wamevaa makoti marefu na walipojaribu kuwasimamisha ili kuwahoji wawili kati yao walitoa silaha na kuanza kuwashambulia polisi.

Alisema polisi walikabiliana na watu hao na kuwajeruhi wawili kati yao, huku wengine wakikimbia na kutokomea gizani.
Alisema waliojeruhiwa walifariki dunia wakiwa njiani kupelekwa hospitalini kwa matibabu.

Kamanda Sabas alisema baada ya kuwapekua watu hao walikuta bunduki mbili aina ya shotgun yenye namba L814574 na CAR 69390 Pump Action ambayo ilikuwa ikimilikiwa na kituo cha afya cha Tumaini kinachomilikiwa na masista.

Alitaja bunduki nyingine kuwa ni yenye namba TZ CAR 39046 na waliokota kofia iliyokuwa na risasi nane za shotgun.
Alisema bunduki zote mbili zilikuwa zimekatwa vitako na mtutu.

Kamanda Liberatus hakuweza kuwataja marehemu hao na maiti zao zimehifadhiwa hospitali ya Mount Meru ya Mkoa wa Arusha kwa utambuzi.

Habari Kubwa