Majambazi yavamia maduka matano Dar, yapora mali

24Feb 2016
Elizaberth Zaya
Dar
Nipashe
Majambazi yavamia maduka matano Dar, yapora mali

WATU wanaodaiwa kuwa majambazi wamevamia maduka matano katika mtaa wa Kimara Temboni, Kinondoni, jijini Dar es Salaam na kupora fedha na mali mbalimbali pamoja na kujehuri watu wawili kwa risasi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime.

Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana, wakati majambazi hao walipovamia eneo hilo wakiwa katika pikipiki mbili na gari mbili, huku wakiwataka wateja na wauzaji waliokuwa katika maduka hayo kulala chini.

Maduka yaliyovamia ni la huduma ya M-pesa, Tigo-pesa, Airtel-money, duka la bidhaa mbalimbali (min super market), duka la vipodozi, duka la vyombo na la nyama.

WALIOVAMIWA WAHADITHIA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Nipashe katika eneo hilo, wauzaji wa maduka hayo walisema majambazi hao walifika saa 2:00 usiku na kutumia kama dakika 20 kukamilisha tukio hilo.

Mmiliki wa duka la mini supermarket, Rogath Shirima, alisema majambazi hao walijigawa katika maduka tofauti waliyovamia na katika duka lake waliingia wawili wakiwa na silaha na kuwaamrisha watu waliokuwapo walale chini na kuwataka watoe fedha.

Alisema ndani ya duka hilo alikuwapo yeye, mke wake, ndugu zake wawili na wateja watatu na baada ya kuamriwa kutoa fedha waliamua kutoa kuokoa uhai wao.

Alisema kabla ya majambazi hayo kutoka katika duka hilo baada ya kupatiwa fedha, waliwapiga yeye na mke wake na stuli na walipotoka nje walipiga risasi mlangoni ambayo ilitoboa mlango na kuwafikia wateja wawili waliokuwa wamelala chini na kuwajeruhi vibaya.

Naye Riberatus Nicolaus, mmiliki wa duka la vipodozi, alisema katika duka lake waliingia majambazi wawili na kumtaka atoe fedha na alipowapatia waliondoka na kwamba wakati hayo yakiendelea dukani kwake, majambazi wengine nje walikuwa wamewaamuru watu waliokuwa wanapita njiani kulala chini na kuwapora.

MAJERUHI
Nipashe jana ilitembelea majeruhi wa tukio hilo ambao walikuwa wamelazwa katika hospitali ya Bochi, Kimara na kushuhudia wakiwa wanapatiwa matibabu.

Mganga wa hospitali hiyo, Dk. Patrick Mbanga, alithibitisha kupokea majeruhi hao, ambao ni Dora Mkoro na Innocent Shirima, usiku wa kuamkia jana.

Alisema mmoja alipokelewa akiwa na hali mbaya akiwa anavuja damu nyingi, hivyo kulazimika kwanza kuzuia hali hiyo kabla ya kumpatia huduma yoyote.

Alisema katika maelezo yao walimwambia kwamba risasi moja ndiyo iliyowajeruhi wote wawili na kwamba katika vipimo walibaini kuwa risasi hiyo ilikuwa kwa mmoja na kwamba hakuna aliyevunjika kiungo zaidi ya nyama za mwili wa mmoja kumeguka kidogo.

POLISI WANENA
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Christopher Fuime, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba baada ya kupewa taarifa walifika usiku huo huo eneo la tukio na kubaini kwamba duka lililokuwa limevamiwa na kupigwa risasi ni moja na watu waliojeruhiwa ni wawili.

Habari Kubwa