Majangili wabadili mwelekeo wageukia kakakuona

24May 2019
Salome Kitomari
DAR
Nipashe
Majangili wabadili mwelekeo wageukia kakakuona

MAJANGILI wa wanyamapori wamebadili mwelekeo na sasa wanawinda kakakuona, ambaye magamba yake husafirishwa kwa ajili ya kutengenezea dawa mbalimbali ikiwamo kuongeza nguvu za kiume.

kakakuona.

Akizungumza na Nipashe jana jijini Dar es Salaam, mtaalamu wa usimamizi wa maliasili na sera wa Shirika la Misaada la Watu wa Marekani (USAID), Exper Pius, alisema hali hiyo imetokana na serikali kuimarisha sheria, sera, kanuni na kukabili mbinu za biashara ya meno ya tembo na pembe za ndovu.

Alisema biashara hiyo ndiyo inashika kasi duniani baada ya soko la meno ya tembo na pembe za ndovu kushuka thamani duniani, kutokana na nchi nyingi Tanzania ikiwamo kubana mianya ya biashara hiyo.

Pius alisema mwaka jana zaidi ya tani 14,000 za magamba ya kakakuona 36 kutoka Nigeria zilizokamatwa Singapore, na kwamba kasi ya biashara hiyo inazidi kuongezeka.

“Kwa Tanzania hakuna takwimu za idadi ya kakakuona au biashara hiyo kama ipo, lakini ni lazima kuchukua tahadhari kwa kuwa ndiyo biashara inayokuwa sana duniani kwa sasa baada ya kuwapo kwa udhibiti mkubwa wa biashara ya meno ya tembo na pembe za ndovu,” alisema.

Alisema biashara hiyo imeshamiri kwenye nchi za Afrika Magharibi, na kwamba kinachofanyika ni kuyatoa na kuyasaga magamba kwa kile kinachoelezwa ni kutengeneza dawa za kuongeza nguvu za kiume na maradhi mengine.

Pia, hutumika kutengeneza mapamba kwa ajili ya matajiri kutoa zawadi kwa watu mbalimbali, na kwamba huhesabika kuwa ni matajiri kama wataweza kutoa zawadi ya magamba ya kakakuona.

Aidha, alisema takwimu zinaonyesha biashara ya meno ya tembo imepungua kwa kiasi kikubwa nchini, na kwamba hatua ya serikali kuimarisha mifumo na kuwachukulia hatua vinara wa biashara hiyo.

Kwa mujibu wa Pius, takwimu zinaonyesha mwaka 2009 hadi 2013 asilimia 60 ya tembo waliuawa, na kati ya 142,785 waliokuwapo waliobakia ni 50,300.

Alisema awali biashara ya meno ya tembo na pembe za faru ilishika kasi kutokana na usimamizi dhaifu wa sheria na faini ndogo ambazo ziliwafanya wenye fedha kuzilipa kirahisi.

“Biashara hii inahusishwa kwa namna moja au nyingine na suala la ugaidi kwa kuwa wanauza pembe za ndovu na meno ya tembo wanapewa silaha, mfano ni nchini Congo ambako wanapeleka nyara hizo na kupata magari yenye silaha,” alisema.

Kwa mujibu wa Pius, pia biashara hiyo inahusiana na biashara ya fedha chafu na kwamba ilikuwa ngumu kuidhibiti kutokana na wanaofadhili kuwa na nguvu kutokana na fedha zao.

“Biashara hii inafanywa na watu wenye fedha nyingi sana ambao hawapo hapa nchini, wanatoa fedha kufadhili hatua zote hadi kufika bandarini na nchi husika. Lakini kwa sasa tangu China imepiga marufuku biashara hiyo soko la meno na pembe imeshuka duniani,” alibainisha.

Asilimia 32 ya eneo la nchi ya Tanzania ni ardhi iliyohifadhiwa, vilima vilivyohifadhiwa 25, maeneo yaliyochini ya hifadhi ya jamii (WMAs) yapo 38.

Aidha, Tanzania ina jumla ya hifadhi za taifa 21 zilizopo chini ya Shirika la Hifadhi ya Taifa (Tanapa) na kwa ujumla utalii unachangia asilimia 17 ya Pato la Taifa (GDP) inatokana na utalii na asilimia 25 ya fedha za kigeni zinatokana na utalii.

Alisema asilimia 80 ya utalii nchini ni wa wanyamapori, huku eneo la utalii wa asili halijafanyika inavyotakiwa.

Habari Kubwa