Majengo Shule ya Ashira kukarabatiwa wiki 3

28May 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Majengo Shule ya Ashira kukarabatiwa wiki 3

BUNGE limeelezwa kuwa tayari serikali imeshapeleka wahandisi katika Shule ya Wasichana Ashira iliyopo mkoani wa Kilimanjaro, ili ndani ya wiki tatu ukarabati wa majengo yake yaliyoungua kwa moto hivi karibuni ufanyike.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo.

Hayo yalielezwa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo, alipokuwa akijibu swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo.

Katika swali lake, mbunge huyo alisema pamoja na juhudi za serikali kuhakikisha kwamba wanajenga mabweni, lakini baadhi ya mabweni hayo yamekuwa yakiungua mara kwa mara.

"Hivi karibuni Shule ya Ashira mabweni yake mawili yameungua, je, serikali mna mpango gani kuhakikisha kwamba kunakuwa na ulinzi katika shule hizo ili rasilimali kubwa ya fedha iliyowekwa ilindwe?" Alihoji.

Akijibu swali hilo, Waziri Jafo alisema juzi alikuwa Shule ya Ashira na kwamba taarifa ya awali inaonyesha ni hujuma.

"Mabweni haya hayajaungana na sio kwamba kulikuwa na hitilafu ya umeme," alisema.

Alieleza kuwa juzi serikali imeshatuma timu ya wahandisi tangu jana inafanya kazi lengo kubwa ndani ya wiki tatu waanze ukarabati wa majengo hayo.

"Ukarabati uanze kwa kuwa muda si mrefu vijana wa kidato cha tano wataingizwa kwenye majengo hayo na tutafanya ukarabati wa shule hiyo yote kwa ujumla wake ili kurudi katika hali yake ya kawaida," alisema.

Kuhusu kuweka ulinzi, alisema "Kipaumbele chetu suala la ulinzi tutahakikisha kunakuwa na ulinzi tunatumia fedha nyingi sana, haiwezekani watu wakahujumu jitihada hizo za serikali." Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum(CCM), Azza Hamad, alihoji mkakati wa serikali wa kujenga mabweni katika shule za sekondari zilizoanzishwa ili kuwasaidia watoto wa kike waweze kupata elimu iliyo bora mkoani Shinyanga.

Waziri Jafo akijibu swali hilo, alisema serikali inatambua umuhimu wa shule za sekondari kuwa na mabweni ili kuboresha elimu na kwa sasa mpango wa serikali ni kuziboresha shule za sekondari zilizopo.

Alisema ukarabati wa shule hizo unahusisha miundombinu ya mabweni hasa kwa watoto wa kike ili waweze kupata elimu iliyo bora.

"Hadi sasa shule za sekondari 1,241 zimejengwa mabweni kati ya 3,634 zilizopo kwa kutumia ruzuku ya serikali kuu, mapato ya ndani ya halmashauri na mchango wa jamii na serikali itaendelea kujenga mabweni kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kadiri itakavyoruhusu," alisema.

Habari Kubwa