Majeruhi ajali ya moto Shule ya Byamungu Islamic waamishiwa Bugando

15Sep 2020
Lilian Lugakingira
Kyerwa
Nipashe
Majeruhi ajali ya moto Shule ya Byamungu Islamic waamishiwa Bugando

Majeruhi wanne kati ya sita waliojeruhiwa katika tukio la moto usiku wa kuamkia jana katika Shule ya Msingi Byamungu Islamic waliokuwa wamelazwa katika Hospitali ya Nyakahanga wilayani Karagwe, wamehamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda, Bugando iliyoko jijini Mwanza.

Akizungumzia hali za majeruhi hao leo Septemba 15,2020 Muuguzi Kiongozi Wodi ya Watoto katika Hospitali ya Nyakahang, Theophilda Ndibalema amewataja waliohamishiwa Hospitali ya Bugando leo kuwa ni Lukumani Said Ramadhan (7), Imani Majaliwa Hatuna (12), Hashraph Mohamed (7) na Juma Seif Juma (12).

Pia ametaja majeruhi wawili waliobaki katika hospitali hiyo ya Nyakahanga kuwa Avitus Sperius (8) na Swabrudin Swaibu (11).

Mzazi wa mtoto Avitus anayeitwa, Sperius Bernard amesema alipata taarifa na kufika shuleni saa 9 usiku lakini alipofika alikuta tayari mtoto wake amepelekwa Hospitali ya Nyakahanga, na kuwa ana imani atapona na kurejea katika hali yake ya kawaida.

Shule ya Msingi Byamungu Islamic iliyoko Kata ya Itera wilayani Kyerwa, imeteketea kwa moto usiku wa kuamkia jana Septemba 14 na kusababisha vifo vya wanafunzi kumi na majeruhi sita.

Habari Kubwa