Maji kuwakomboa wasichana sekondari

14Feb 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe Jumapili
Maji kuwakomboa wasichana sekondari

WANAFUNZI wa kike wanaosoma katika Shule ya Sekondari Masengwa, wilayani Shinyanga, wanatarajia kuondokana na adha ya kukatisha masomo yao kwa ujauzito kutokana na kufuata maji umbali mrefu, baada ya mradi wa maji kutoka Ziwa Victtoria kuelekezwa shuleni huko.

Eta Elisoni, mwanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo, alibainisha matarajio yao hayo juzi wakati Bodi ya Wazabuni ya Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) mkoani Shinyanga, ilipokagua utekelezaji wa miradi ya maji ya Ziwa Victoria katika Kijiji cha Masegwa inakopatikana shule hiyo.

Alisema katika shule hiyo, wanafunzi wa kike huwa wanaishi bwenini, lakini kikwazo kikuu cha maendeleo yao kielimu ni kufuata maji umbali wa takriban kilomita moja kutoka shuleni na kwamba huko njiani hukutana na vishawishi na kujikuta baadhi yao wakiacha masomo kwa kupewa ujauzito.

"Wasichana ambao tuanaishi hosteli hapa shuleni huwa tunakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji, na tunapofuata maji kijiji jirani cha Mwamatongo, hukumbana na vishawishi vya kutongozwa kila siku na baadhi yetu hupata ujauzito na kuacha masomo," aliwasilisha kilio chao.

Mkuu wa Shule hiyo, Salu Mlyambate, alisema tatizo la ukosefu wa maji shuleni hapo limekuwa kikwazo kitaaluma kwa wanafunzi wa kike ambao wanaishi bwenini kwa kuwa hupoteza muda wa masomo kufuata maji na wengine kuingia kwenye uhusiano ya kimapenzi na wanakijiji.

Meneja Wakala wa Maji Vijijini (Ruwasa) mkoani Shinyanga, Julieth Payovela, alisema mradi huo wa maji katika Kijiji cha Masengwa, unatarajiwa kukamilika Februari 28, mwaka huu na kusambaza maji kijijini huko zikiwamo taasisi za serikali, ukigharimu Sh. milioni 234.

Habari Kubwa