Majibu kero za walimu Alhamisi

07Dec 2017
Romana Mallya
Nipashe
Majibu kero za walimu Alhamisi

WALIMU wanaamini kuwa majibu ya kero zao mbalimbali zinazowakabili yatapatikana Alhamisi ijayo baada ya Rais John Magufuli kupanga kuzungumza nao kupitia Mkutano Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).

Mkutano huo uliokuwa ufanyike mkoani Arusha, sasa utafanyika mjini Dodoma kwa ajili ya kumpa fursa Rais Magufuli kufika mkutanoni.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, makamu wa rais wa CWT, Leah Ulaya alisema siku hiyo itakuwa fursa ya pekee kwa Rais Magufuli kuzungumza na walimu na kujibu hoja zinazowatatiza.

Ulaya alisema baada ya Rais Magufuli kupata taarifa za kufanyika kwa mkutano huo mjini Arusha, ndipo alipoona ni vyema apate nafasi ya kuzungumza na walimu.

"Rais Magufuli ameona ni vyema kuzungumza na walimu kupitia Mkutano Mkuu wa CWT ambao utafanyika kwa siku mbili kuanzia Alhamis ijayo," alisema Ulaya na kwamba "chama kilimuomba awe mgeni rasmi na amekubali.

"Baada ya kukubali (kuwa mgeni rasmi) ameomba mkutano ufanyike Dodoma kwa sababu siku hiyo atakuwa na shughuli nyingine za kitaifa mjini humo, itakuwa rahisi kushiriki mkutano wetu."

Ulaya alisema kwa Rais Magufuli kuhudhuria mkutano huo wanaamini ataweza kuzitolea ufafanuzi wa jumla hoja mbalimbali za walimu kwa sababu ndiye mwajiri mkuu.

"Hii itakuwa ni mara ya kwanza Rais Magufuli kuwahutubia walimu kupitia mkutano mkuu na kutimiza jambo kubwa la kutekeleza na kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere kwa kuhamia Makao Makuu Dodoma."

Aidha, kiongozi huyo aliwataarifu washiriki wa mkutano huo ambao tayari walikuwa wamejiandaa kwa safari ya Arusha kuwa sasa waelekee Dodoma.

Katika hatua nyingine, Ulaya alisema baada ya Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kuagiza zoezi la kupandisha madaraja lianze Novemba 1, mwaka huu, baadhi ya maswali yaliibuka.

Alisema miongoni mwa maswali hayo ni yale yaliyohusu madaraja na vyeo vianze kuhesabiwa kuanzia Novemba mosi wakati usitishwaji ulianza mwezi Juni, mwaka jana.

"Maswali mengine yalihusu walimu waliopandishwa madaraka kati ya Februari na Aprili mwaka jana hatima ya mapunjo yao ikoje; hasa baada ya agizo hilo la madaraja na vyeo kuanza Novemba mosi," alisema Ulaya.

Pia alisema walimu wanahoji kuhusu wastaafu baada ya kupata madaraja na vyeo vipya.

"Hoja iliyokuja ilihusu madaraja na vyeo kuhesabika kuanzia Novemba mosi na vipi kuhusu barua walizopewa kama zitakuwa na maana yoyote," alisema.

Alisema baada ya sintofahamu hiyo kwa walimu, Novemba 28, viongozi wa CWT walikutana na Katibu Mkuu Utumishi ili kupata ufafanuzi kuhusu maswali hayo ndipo alipowataka waandike barua.

"Katibu Mkuu Utumishi alikubali ombi la uongozi wa CWT na alitutaka tuweke hoja zetu kwa maandishi tumefanya hivyo na tumewasilisha serikalini na sasa tunasuburi majibu," alisema.

Habari Kubwa