Majibu ya TAKUKURU hoja 10 za CHADEMA

04Jul 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Majibu ya TAKUKURU hoja 10 za CHADEMA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imejibu hoja 10 za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu chama hicho kutokuwa na imani na uchunguzi unaofanywa na taasisi hiyo dhidi yake.

KATIBU MKUU WA CHADEMA, JOHN MNYIKA:PICHA NA MTANDAO

Mwezi uliopita, TAKUKURU ilitangaza kuanza uchunguzi kuhusu tuhuma za matumizi mabaya ya michango ya wanachama wa CHADEMA, wakiwamo wabunge wake wanaokatwa sehemu ya mishahara yao ili kutunisha mfuko wa chama.

Hata hivyo, juzi, CHADEMA kupitia kwa Katibu Mkuu wake, John Mnyika, ilisema haina imani na uchunguzi unaoendelea kufanywa na taasisi hiyo dhidi yake kutokana na kauli alizoziita za kisiasa zilizotolewa na uongozi wa juu wa TAKUKURU kuhusiana na uchunguzi huo.

Mnyika alisema taasisi hiyo tayari imeshawahoji watu 60, wakiwamo viongozi na wanachama wa CHADEMA huku pia wakiikabidhi nyaraka kadhaa zinazohusiana na fedha za michango ya wabunge wa chama hicho.

Mnyika alidai uchunguzi huo unafanywa kisiasa kwa lengo la kuichafua CHADEMA kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu, huku akisisitiza kwamba hadi sasa TAKUKURU haijaweka wazi ukomo na aina ya tuhuma ambazo zinaikabili CHADEMA.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, Ofisa Uhusiano wa TAKUKURU, Doreen Kapwani, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wake, Brigedia Jenerali John Mbungo, alijibu hoja 10 za chama hicho.

Alianza kujibu hoja ya CHADEMA kutokuwa na imani na uchunguzi wa TAKUKURU, akisema taasisi hiyo ni chombo cha uchunguzi kilichoundwa na kupewa mamlaka ya kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007.

“Sheria hii ilipitishwa na wabunge, wakiwamo wa Chadema, hivyo wote wanafahamu lengo na madhumuni ya kuanzishwa kwa chombo hiki pamoja na mamlaka yake kisheria katika kuongoza mapambano dhidi ya rushwa nchini," alisema.

Kapwani pia alisema TAKUKURU ni chombo chenye wataalamu waliobobea katika shughuli za kiuchunguzi na kamwe hakiwezi kuelekezwa namna ya kufanya uchunguzi dhidi ya tuhuma za rushwa na watu ambao kinawachunguza.

“Hiki ni chombo huru kwa mujibu wa kifungu cha 5(2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007,” alisema.

Kuhusu hoja ya ukomo wa uchunguzi, Kapwani alifafanua kuwa kitaaluma, suala la uchunguzi huwa halina mipaka wala ukomo, hivyo wakichunguza jambo moja, hawawezi kuzuiwa kuchunguza jambo lingine linalojitokeza katika uchunguzi huo.

“Kupitia taarifa hii, tunawaomba Chadema waendelee kutoa ushirikiano wanaopaswa kuutoa kwa TAKUKURU kwa sababu kutofanya hivyo ni kinyume cha matakwa ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007,” alisema.

Kapwani alisema CHADEMA wanapaswa kutulia na kusubiri matokeo ya uchunguzi kwa sababu kupitia uchunguzi wowote, ukweli hujulikana na uongo hubainika.

Kuhusu taasisi kutumika kisiasa, Kapwani alisema hoja hiyo haina msingi kwa kuwa TAKUKURU ni chombo huru kinachotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na mamlaka yake ni kuchunguza bila ubaguzi wowote wa rangi, dini, kabila, chama, jinsi, umri wala elimu.

Alisema inafahamika kuwa CHADEMA ndiyo chama kilichosimama bungeni kupitia wabunge wake na kutoa malalamiko dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za michango yao na ubadhirifu ni kosa la jinai.

"Malalamiko yale yalikuwa ni chanzo cha taarifa kwa TAKUKURU na hata kama suala kama hilo lingetokea kwa chama kingine chochote, taasisi ingefanya hivyo hivyo,” alisema.

Kapwani alikiri tuhuma hizo zimeibuka kipindi ambacho nchi inaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa viongozi Oktoba mwaka huu, lakini akasisitiza kuwa tuhuma za jinai zinapotokea, haziwezi kuachwa kwa kisingizio cha kuwa kwenye kipindi cha uchaguzi.

Kuhusu hoja ya TAKUKURU kuhoji wabunge wa CCM juu ya madai ya ubadhirifu ndani ya CHADEMA, Kapwani alisema haina msingi kwa sababu wanaongozwa na tuhuma zinazochunguzwa.

Alitoa wito kwa CHADEMA kusoma vifungu vya 5,7 a, b, c, d, e, f na g pamoja na kifungu cha 28(ii) vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007, ili kufahamu mamlaka ya TAKUKURU na sababu ya kuchunguza suala hilo.

Habari Kubwa