Majibu ya waziri madai fidia wakazi Kipunguni

02Jul 2019
Beatrice Moses
Dar es Salaam
Nipashe
Majibu ya waziri madai fidia wakazi Kipunguni

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe, amesema suala la fidia za wakazi wa Kipunguni jijini Dar es Salaam wanaopaswa kuhama ili kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege ni la kisheria.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe.

Maelezo ya waziri huo yanatokana na swali aliloulizwa na gazeti hili jana kuhusu mkutano ulioandaliwa ili azungumze na wakazi wa Kipunguni Jumamosi, lakini hakufika ikidaiwa alipata dharura, hivyo kwenda bandarini.

Wakazi hao walicharuka mbele ya Mbunge wa Segerea, Bonna Kamoli, aliyeandaa mkutano huo, wakimjulisha kuwa wanamhitaji waziri huyo ili hawajulishe ni lini watalipwa fidia zao wanazodai kwa zaidi ya miaka 20.

“Suala unaloniulizia ni la kisheria, kama unahitaji ufafanuzi andika barua kwa Katibu wa Wizara,” alisema Waziri Kamwele.

Mhandisi Kamwelwe ni Waziri wa Wizara hiyo tangu Julai 2018 ambapo mtangulizi wake ni Prof. Makame Mbarawa, aliyehamishiwa Wizara ya Maji.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kipunguni, Praxeda Mkandara, aliwatangazia wananchi hao kuahirishwa kwa mkutano huo hadi watakapoarifiwa tena.

Alieleza kuwa taarifa walizonazo ni kwamba waziri amepata dharura amekwenda Bandari ya Dar es Salaam kuna tishio la mgomo wa madereva.

Mwenyekiti huyo aliliambia gazeti hili kuwa tatizo hilo limekuwa ni kero kubwa kwa wananchi, limedumaza maendeleo yao huku baadhi ya wananchi wa Kipunguni Mashariki wakiamua kuendelea na ujenzi wa nyumba zao wakitarajia kufanyiwa tathmini.

“Ni kero kwa wananchi bora waambiwe ukweli maana jambo hili limeshughulikiwa na mawaziri karibu wanne, lakini hadi sasa hakuna suluhisho, mbunge wa upande wake amekuwa akijitahidi kukumbusha jambo hili lishughulikiwe,” alisema.

Wakazi wa Kipunguni kwa nyakati tofauti wamekuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa ulipaji wa fidia hiyo, hatua ambayo imewafanya wengi washindwe kuyaendeleza maeneo hayo wakihofia kuhamishwa wakati wowote.

Mmoja wa wakazi hao, Hilda Kaijage, alisema ucheleweshwaji wa malipo ya fidia hiyo umewakwamisha kimaendeleo kwa kuwa imechukua miaka mingi bila kutolewa, pia wamekuwa wakiishi kama wapo kizuizini.

Mkazi mwingine, Mustafa Ahmed, anakumbuka wakati anajenga nyumba yake yenye vyumba sita saruji ilikuwa inauzwa shilingi 3,800 ikichangazwa na gharama za nauli ilikuwa 200 kwa mfuko mmoja.

Mbunge Kamoli alieleza kuwa jambo hilo la fidia limekuwa likimkosesha amani kwa kuwa anatambua ni haki ya wananchi hao kulipwa ili wajiendeleze kimaisha katika maeneo waliyopewa.