Makada CHADEMA wachukua fomu urais

09Jul 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Makada CHADEMA wachukua fomu urais

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu, amekuwa mtia nia wa nne kuchukua fomu ya kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwa tiketi ya chama hicho.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Regnal Munisi (kulia), akikabidhi fomu ya kuwania kuteuliwa kugombea urais kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Kanda ya Kati, Lazaro Nyalandu, jijini Dar es Salaam, jana. PICHA: JUMANNE JUMA

Wakati Nyalandu ambaye aliwahi kuwa Waziri katika serikali ya awamu ya nne akijitokeza, kada mwingine wa chama hicho, Wakili Gasper Mwanalyela, pia amejitosa katika kinyang’anyiro hicho.

Nyalandu amesema endapo atachaguliwa kupeperusha bendera kupitia chama hicho, aterejesha uhuru wa mihili ya Bunge, Mahakama na Utawala (Serikali) na kwamba anatamani Tanzania iliyo tofauti na ya sasa, isiyogawanyika na isiyo na fursa ya kuwagawanya Watanzania kimakundi.

Kauli hiyo aliitoa jana wakati akikabidhiwa fomu hiyo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CHADEMA, Reginald Munisi, katika Makao Makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam.

Alisema anatamani kuiona Tanzania inayoongozwa na Katiba mpya, itakayodadavua na kurekebisha mifumo iliyoanza kuyumba kutokana na baadhi ya watu walioanza kuichakachukua kutokana na udhaifu wa mifumo hiyo.

“Wakati naondoka CCM nilisema ili nchi iwe sawa sawa ni lazima Serikali, Mahakama na Bunge viwe huru. Haya mafiga matatu yanatakiwa yajitegemee na yajiendeshe pamoja. Tunataka nchi ambayo mwananchi akikosewa na serikali yake awe na uhuru wa kuipeleka mahakamani,” alisema.

Nyalandu ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika Serikali ya Awamu ya Nne, alisema atarejesha umoja wa kitaifa na kuondoa tofauti za kisiasa.

“Jambo la kwanza ni kuhakikisha tunarejesha umoja wa kitaifa. Matumaini ya Watanzania ya udugu, upendano na ushirikiano, penye lawama tupeleke upendo. Nilipokuwa CCM nilimshika mkono (Freeman) Mbowe (Mwenyekiti wa CHADEMA) na tukafanya kazi. Umoja ule wa kitaifa upite tofauti zetu tunazoziona,” alisema Nyalandu.

WAKILI MWANALYELA

Awali, Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania, Mwanalyela, alikuwa mwanachama wa tatu kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea urais wa Tanzania kupitia CHADEMA, huku akitanabahisha kuwa ameamua kugombea ili kurudisha matumaini kwa wananchi walio na hofu na wenye kukata tamaa.

Pia alisema atafuata nyayo za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, za kuanzisha vijiji vya ujamaa na kujitegemea na kwamba, atakwenda mbali zaidi kwa kuanzisha vijiji vya wataalamu.

“Baba wa Taifa alianzisha vijiji vya ujamaa na kujitegemea. Tunapaswa kutengeza vijiji vya wataalamu wa madaktari, teknolojia na kilimo. Vijiji hivi ni muhimu kuongeza ugunduzi na uvumbuzi,” alisema.

Alisema endapo atateuliwa na CHADEMA kugombea urais na kisha kuchaguliwa na wananchi kuwa Rais wa Tanzania, atahakikisha Katiba ya wananchi inapatikana, pamoja na kutoa elimu ya uraia kwa wananchi ili wajue haki na majukumu yao katika Taifa.

Pia alisema suala hilo litakwenda sambamba na upatikanaji Katiba ya wananchi, kwa sababu ndani ya Katiba, mkataba wa kijamii unapatikana na kwamba ataufumua mfumo wa ulinzi na usalama, elimu, biashara, kilimo, teknolojia ili sekta hizo ziendane na mabadiliko ya sasa.

Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, alikuwa wa kwanza kuchukua fomu Julai 4, kupitia wakala wake David Jumbe. Dk. Mayrose Majinge alikuwa wa pili kwa kuchukua fomu juzi.

Kuanzia Julai 22 mwaka huu, Kamati Kuu ya CHADEMA itapendekeza jina la mgombea urais na Julai 29 mwaka huu, mkutano mkuu wa CHADEMA utapitisha jina la mgombea wa urais wa Tanzania Bara.

Habari Kubwa