Makamba asema ujumbe umefika

17Jul 2019
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Makamba asema ujumbe umefika

KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba, amesema wanaamini ujumbe wa tamko lao la mwishoni mwa wiki umefika kwa walengwa.

KATIBU Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yusuph Makamba.

Amesema hata kama Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM halitajibu malalamiko yao, tamko lao lililenga kuujulisha umma kuwa hawahusiki kwa namna yoyote na tuhuma zinazotolewa dhidi yao.

Julai 14, mwaka huu, Makamba na Abdulrahman Kinana ambaye pia ni katibu mkuu mstaafu wa CCM, walitoa tamko la kufafanua tuhuma zilizoelekezwa kwao na mtu aliyejitambulisha kuwa ni mwanaharakati.

Katika tamko hilo, wawili hao walisema tathmini ya awali inaonyesha mtu huyo anatumiwa kusambaza taarifa hizo zinazolenga kuwadhalilisha, kuwachafua na kuwashushia heshimu mbele ya jamii.

Akizungumza na Nipashe jana, Makamba alisema walishiriki kumweka madarakani Rais na serikali iliyoko madarakani, hivyo tuhuma zinazoelekezwa kwao hazina mashiko.

“Inawezekana hamjaelewa lengo la tamko letu, hatukulielekeza kwa baraza, bali kutoa taarifa kwao (baraza), umma na wanaCCM kuwa sisi hatuhusiki, ni watu safi,” alisema.

Makamba aliongeza: "Sisi ni watu safi, hatuhusiki na jambo lolote, hiyo kazi tumeimaliza, sisi ni watu safi, maneno yanayosemwa juu yetu ni uzushi, hatuhusiki na hizo tuhuma, serikali tuliitafuta sisi na tulishiriki kumweka Rais madarakani, baraza lijibu lisijibu. sisi tumemaliza kazi yetu."

Katika tamko lao, Makamba na Kinana walisema walimwandikia barua Katibu Mkuu wa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, Pius Msekwa, kulishauri litumie busara katika kushughulikia jambo hilo linaloelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu wa chama hicho.

Baraza hilo liko chini ya uenyekiti wa Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye pia ni mwenyekiti mstaafu wa CCM.

Walisema wameamua kutokwenda mahakamani kwa sababu kuu mbili ambazo walizitaja kuwa ni pamoja na jambo lenyewe kuwa na taswira ya kimkakati na lina mtandao wenye malengo ya kisiasa, hivyo linapaswa kushughulikiwa kisiasa.

Walisema sababu ya pili kutoona kiwango cha fedha ambacho kinaweza kulipwa na kikawiana na heshima yao.

Kauli za mwanaharakati huyo, walisema zinaonyesha si zake bali anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipaza sauti na kwamba ni mamluki anayetumika kuivuruga CCM na nchi kwa ujumla.

Katibu wa baraza hilo, Msekwa, alikaririwa jana akisema suala la viongozi hao limeshapelekwa katika ngazi za juu, huku kukisambaa katika mitandao ya kijamii taarifa iliyodaiwa kutolewa na Spika mstaafu huyo kuhusu majibu ya awali ya baraza kwa Kinana na Makamba.

Hata hivyo, Msekwa hakupokea simu alipotafutwa na Nipashe jana kuzungumzia taarifa hiyo.