Makamu wa pili wa Rais wa Z’bar awataka wasimamizi SNR kuongeza kasi

10Jun 2021
Na Mwandishi Wetu
Zanzibar
Nipashe
Makamu wa pili wa Rais wa Z’bar awataka wasimamizi SNR kuongeza kasi

​​​​​​​MAKAMU wa pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, amewataka maafisa wanaosimamia mfumo wa sema na Rais Mwinyi (SNR) kuongeza kasi katika kutoa majibu ya malalamiko kutoka kwa Wananchi.

Abdulla amesema hayo katika kikao alichoketi na Watendaji wakuu wa Wizara, Makamanda pamoja na Maafisa wanaosimamia mfumo huo katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdull-wakili kikwajuni jijini Zanzibar.

Abdulla amewaeleza wasimamizi hao kuwa mfumo uliozinduliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha mfumo huo unafanya kazi vizuri ili lile lengo la serikali la kuwahudumia wananchi wake liweze kufikiwa.

Amesema Wananchi wamekuwa na muamko mkubwa katika kuutumia mfumo huo kwa kutuma malalamiko na changamoto zinazowakabili lakini bado kumekuwepo na changamoto ya maafisa hao kutotoa majibu kwa wakati muwafaka jambo linalosababisha usumbufu kwa Wananchi kwa kuona hakuna hatua zianazochukuliwa na taasisi zinazosimamia majukumu yao.

Aidha, Makamu huyo ameonesha kufurahishwa na kasi ya kiutendaji inayochukuliwa na makatibu wakuu katika kutoa ushirikiano kwa maafisa hao wanaosimamia mfumo wa sema na Rais Mwinyi (SNR) hasa katika kutatua changamoto zinazowaakabili maafisa hao akitolea mfano changamoto ya upatikanaji wa bando na vocha kwaajili ya wanasiliano.

Habari Kubwa