Makamu wa sekondari atumbuliwa Songea

05Mar 2016
Gideon Mwakanosya
Nipashe
Makamu wa sekondari atumbuliwa Songea

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, amemvua madaraka na kumhamisha makamu mkuu wa shule ya sekondari Namabengo wilayani Namtumbo, Shaibu Chanpunga.

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu

Mkuu huyo alikuwa akituhumiwa na wanafunzi wa shule hiyo kwa lugha chafu na vitendo vya udhalilishaji kwa kuwachapa viboko visivyokuwa na idadi kinyume na sheria za nchi.

Akizungumza na Nipashe ofisini kwake jana, Mwambungu alisema amechukua uamuzi wa kumvua madaraka na kumhamisha makamu mku wa shule Champunga juzi alipokwenda kusikiliza kero za wanafunzi.

Wanafunzi hao walikuwa wameandamana kwa kutembea kwa miguu kutoka Namabengo wilayani Namtumbo, kwenda Songea kwa lengo la kuonana na Mkuu wa Mkoa katikati ya wiki, lakini maandamano hayo yalivunjwa na polisi njiani.

Mwambungu alieleza kuwa aliamua kwenda kwenye shule hiyo kwa lengo la kusikia kilio cha wanafunzi ambao walikuwa wanataka kuonana naye.

Mwambungu alisema kuwa alipofika kwenye shule hiyo alizungumza na wanafunzi wote kwanza, na wakamueleza kero nyingi dhidi ya makamu mkuu wa shule Champunga.

Alisema katika mazungumzo na walimu pamoja uongozi wa shule, ilibainika kuwa Champunga alikuwa na mapungufu mengi amabayo yalimfanya alazimike kumvua madaraka na kumhamisha shule.

Mwambungu ametawaka walimu na uongozi wa shule hiyo kuona umuhimu wa kuzingatia kanuni na sheria pale wanapochukua hatua ya kutoa adhabu kwa wanafunzi .

Wanafunzi 106 wa kidato cha sita wa Sekondari ya Namabengo waliandamana kutaka kutembea kwa miguu umbali wa km 16 Jumanne, lakini walipofika kijiji cha Mlete kilichopo nje kido ya manispaa ya Songea walizuwiwa na polisi.

Habari Kubwa