Makandarasi waelekezwa kutumia malighafi za ndani

22Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
Kahama
Nipashe
Makandarasi waelekezwa kutumia malighafi za ndani

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo, amewataka makandarasi kutumia malighafi za nchini ili kukamilisha miradi inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali kwa wakati.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Prof. Kitila Mkumbo picha na mtandao

Alisema kutumia malighafi kutoka nje kunachelewesha kukamilisha miradi kutokana na kuchelewa kufika.

Aidha, alisema hali hiyo inasababisha wananchi kuchelewa kupata huduma ambao ndio walengwa wa miradi hiyo.

Prof. Mkumbo aliyabainisha hayo juzi wakati akisaini hati ya makubaliano ya kisheria katika kutekeleza mradi wa pamoja unaogharimu kiasi cha Sh. bilioni 13.8 utakaohudumia zaidi ya wananchi 10,000 wa mikoa ya Geita na Shinyanga.

Alisema kila mkandarasi anatakiwa kutumia ipasanyo malighafi kutoka katika viwandani vya ndani, ili iwe rahisi kukamilisha miradi kwa wakati na kutoa huduma kwa wananchi, huku akivitaka viwanda vya ndani kuzalisha malighafi zenye ubora.

“Nataka kuona kila mkandarasi anatumia malighafi kutoka katika viwanda vyetu vya ndani na sio kwenda kununua nchi za nje, tumekuwa tukipoteza muda katika kukamilisha miradi yetu tunayotekeleza kwa kusubiria malighafi kutoka nje, huku viwanda vyetu vinazalisha kila aina ya malighafi,” alisema.

Prof. Mkumbo aliongeza: “Kuna viwanda vyetu vya ndani hakikisheni mnatengeneza bidhaa au malighafi zenye ubora wa hali ya juu.”

Alilitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuhakikisha bidhaa hizo kama zina ubora unaotakiwa kabla ya kuingizwa sokoni.

Aidha kuhusu mradi wa pamoja wa maji, Prof. Mkumbo alisema mradi huo kwa awamu ya kwanza utagharimu Sh. bilioni 13.8, huku Halmashauri ya Shinyanga ikitoa milioni 400, Halmashauri ya Msalala milioni 600, Halmashauri ya Nyang’hwale milioni 600, Acacia Bulyanhuru bilioni 4.5 na Serikali Kuu bilioni 5.2.

Meneja wa migodi ya Bulyanhuru na Buzwagi, Benedict Busunzu, alisema mradi huo utapita katika vijijini 14 kutoka mikoa ya Geita na Shinyanga na kwamba utasaidia kumshusha mama ndoo kichwani ifikapo mwaka 2021.

Meneja mradi wa kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (BCEG), Lzangi Li, alisema asilimia kubwa ya malighafi ambayo ni mabomba atatumia ya viwanda vya ndani na kwamba zaidi ya Sh. bilioni 3.4 zimetegwa kwa ajili ya kununua vifaa hivyo.

Habari Kubwa