Makazi Makamu Rais kugharimu bil. 1.5/-

07Dec 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Makazi Makamu Rais kugharimu bil. 1.5/-

MATENGENEZO kwenye makazi ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan pindi atakapohamia Dodoma yatagharimu Sh. bilioni 1.5, imeelezwa.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

Aidha, imeelezwa pia kazi ya kutenganisha ofisi za watumishi na wasaidizi wa Makamu wa Rais itagharimu Sh. milioni 680.

Gharama hizo zimo katika taarifa ya ujenzi huo ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais ashughulikiae Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Wenye Ulemavu na Vijana, Jenista Mhagama.

Mhagama alisoma taarifa hiyo jana mjini hapa wakati Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua matengenezo ya makazi ya muda yanayotarajiwa kutumiwa na Makamu wa Rais atakapohamia hapa. 

Waziri Mkuu alifanya ukaguzi huo jana katika eneo la Kilimani, mjini Dodoma ambako yalikuwa makazi ya Mkuu wa Mkoa.

Baada ya Rais John Magufuli kutangaza kuwa serikali itahamia Dodoma, Septemba 16, mwaka jana, Majaliwa alitoa ratiba ambapo alisema utekelezaji wa mpango wa serikali kuhamia Dodoma ungekuwa na awamu sita.

Katika ratiba hiyo, Majaliwa alisema awamu ya kwanza ingeanza mwezi huo hadi Februari, mwaka huu huku ya mwisho ikiwa Machi-Juni, 2020.

Mhagama alisema kikosi kazi cha kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma kilibaini kuwa mahali alipokuwa akiishi awali Mama Samia siyo sahihi kwa ajili ya makazi ya kudumu ya Makamu wa Rais.

“Pale (alipokuwa akifikia) palikuwa panafaa kwa ajili ya ziara za kikazi alipokuwa akija Dodoma," alisema Waziri Mhagama, "kwa hiyo tumeamua tufanye ukarabati hapa ili aweze kuishi kwa viwango vinavyostahili.”

Waziri Mkuu pia alikagua matengenezo ya Ofisi inayotarajiwa kutumiwa na Makamu wa Rais ambayo itakuwa eneo la Ndejengwa.

Wakati huohuo, Kaimu Meneja wa Wakala wa Ujenzi (TBA) mkoa wa Dodoma, Steven Simba ambaye anasimamia ujenzi huo, alimweleza Waziri Mkuu kuwa wanataraji kazi hiyo itakamilika kabla ya mwisho wa mwezi.

AWAMU YA PILI

Katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango wa serikali kuhamia Dodoma, Waziri Mkuu, mawaziri wote, makatibu wakuu, manaibu makatibu wakuu na alau idara mbili za kila wizara zimehamia Dodoma.

Baada ya awamu ya kwanza ya ratiba hiyo, awamu ya pili ilikuwa Machi-Agosti, mwaka huu ambapo watendaji mbalimbali wa serikali waliendelea kuhamia Dodoma kwa mafungu.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa katikati ya mwaka jana, awamu ya tatu ingeanza Septemba na kukamilika Februari mwakani na kufuatiwa na awamu ya nne ya Machi-Agosti.

Awamu ya tano ya utekelezaji wa mpango wa serikali kuhamia Dodoma, kwa mujibu wa Majaliwa itakuwa Septemba mwakani mpaka Februari, 2020.

Awamu ya mwisho, ilielezwa na Waziri Mkuu wakati akihitimisha mkutano wa nne wa bunge la 11 itakuwa Machi-Juni, 2020 kwa Rais Magufuli na ofisi yake kuhamia Dodoma. 

Habari Kubwa