Makinda afunda shule kuandaa viongozi

22Oct 2018
Na Mwandishi Wetu
Chalinze
Nipashe
Makinda afunda shule kuandaa viongozi

SPIKA mstaafu Anne Makinda amezitaka shule kuandaa vijana kuwa viongozi bora wa baadaye.

SPIKA mstaafu Anne Makinda.

Aliyasema mwishoni mwa wiki katika mahafali ya kwanza ya kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Imperial (ISS) yaliyofanyika Msolwa, Chalinze mkoani Pwani ambapo alikuwa mgeni rasmi.

Makinda alisema shule zina jukumu la kuwaandaa vijana kuwa viongozi bora kwa kuwa anaamini zenyewe ndiyo chimbuko la viongozi bora.

"Chimbuko la viongozi bora linaanzia shuleni, shule hazina budi kujiandaa kwa hilo," Makinda alisema.

Katika mahafali hayo, Makinda ambaye kwa sasa ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa ya Bima ya Afya (NHIF), alizindua kampeni maalum ya shule hiyo inayoitwa 'Uongozi Bora' kuhamasisha wanafunzi kujiandaa kuwa viongozi wazuri.

Alisema wanafunzi wanapaswa kuaminishwa kuwa wanaweza kuwa viongozi bora tangu wakiwa wadogo, hivyo kujenga tabia ya kujilinda na kujichunga wenyewe.

Makinda alipongeza jitihada za shule hiyo kwa kutambua wajibu huo na kuanzisha kampeni hiyo mapema kwa wanafunzi wake.

"Shule ina mandhari nzuri, naamini viongozi wazuri watatoka hapa," Makinda alisema na kuwashauri wazazi kupeleka watoto wao katika shule hiyo, akieleza kuwa ina viwango vya kimataifa.

Mkuu wa Shule hiyo, Lincolin Mashanda, alisema shule yao imejiandaa kuzalisha viongozi bora wa kesho katika fani na nyanja mbalimbali kwa kuzingatia ubora na maadili mema kwa wanafunzi.

"Yapo mambo kadhaa ambayo yanamfanya mtu awe kiongozi bora," Mashanda alisema "mambo haya yakianza kuzoeshwa mapema huwa tabia na mwongozo kwa vijana wetu.

"Kituo cha Utafiti na Mafunzo ya Uongozi cha Dale Carnegie jijini New York, Marekani, katika utafiti wao wamegundua kwamba kinachomfanya mtu awe kiongozi bora siyo suti wala sura, bali uwezo na nia ya dhati katika kuamsha ari kuwawezesha unaowaongoza wawe bora zaidi, kuwafanya wajiamini na kuwapa motisha.

"Kiongozi bora ni yule anayeweza kuyakabili matatizo au changamoto. Ni yule ambaye ana ujasiri wa kutosha wa kukabiliana na kila aina ya changamoto inayojitokeza kwa busara.”