Makinda asimulia alivyotukanwa matusi

20Mar 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Makinda asimulia alivyotukanwa matusi

SPIKA mstaafu wa Bunge la Tanzania, Anna Makinda, amesimulia alivyotukanwa matusi ya kila aina alipokuwa akiwania nafasi mbalimbali za uongozi na kwamba aliitwa dikteta alipochaguliwa kuwa Spika wa Bunge.

Mwenyekiti wa bodi ya mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya,(NHIF) na Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda akisalimiana na baadhi ya wanawake wajasiriamali jijini Dar es Salaam jana, katika kuiadhimisha siku ya mwanamke Duniani iliyo andaliwa na Shirika lisilo la kiserekali la Umoja wa mataifa unao shughulikia usawa wa kijinsia,(UN WOMEN)ambapo kauli mbiu yake ni “Badili Fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa Maendeleo endelevu”.PICHA: GETRUDE MPEZYA

Makinda aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wanawake wafanyabiashara ndogo ndogo masokoni, wakati wa kuadhimisha siku ya wanawake katika hafla iliyoandaliwa na Taasisi ya Equality For Growth (EFG).

Alisema wanawake hawapaswi kukata tamaa wanapokutana na changamoto za matusi na vitisho wakati wa kuwania nafasi za uongozi au kutekeleza majukumu yao na badala yake wasonge mbele.

“Mimi wakati nagombea nafasi za uongozi nilitukanwa sana lakini sikujali nilisonga mbele. Nikiwa madarakani ilifika wakati nikaitwa dikteta,” alisema Makinda.

Aliwataka wanawake wasijirudishe nyuma katika shughuli wanazofanya kwa kuhofia kusemwa vibaya au kutukanwa bali wasimamie kile wanachokiamini na kufikia malengo yao.

“Nilitukanwa sana hadi yale matusi nikiyakumbuka leo najiuliza hivi ni mimi au ni mtu mwingine? Lakini sikujali nilisonga mbele, hivyo na nyie msiangalie matusi mnayotukanwa leo bali msonge mbele tu,” alisema.

Makinda aliwataka wanawake wajitokeze kwa wingi ukifika wakati wa kuwania nafasi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, uongozi kwenye masoko na kwenye makundi mbalimbali ili washiriki kikamilifu katika ngazi za uamuzi.

Makinda pia aliwataka wanawake hao wajasiriamali wachukue vitambulisho vya wafanyabiashara kwa sababu vitawawezesha kutambulika na kuwa na maeneo rasmi ya kufanyia biashara na kupata mikopo.

Pia aliwataka wanawake hao kujiunga na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa ajili ya kupata matibabu watakapougua na kwamba kutofanya hivyo ni kujiweka katika nafasi ya kurudi nyuma kimaendeleo.

“Siku hizi kuna magonjwa makubwa ambayo matibabu yake ni ghali kama huna bima ya afya, amini kuwa utakapougua wewe au mtoto wako, fedha ulizoweka akiba na mtaji wa biashara utaisha, hivyo kuwa na bima ni kuwa na uhakika wa maisha,” alisema Makinda.

Aliwasihi wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuchangamkia bima ya CHF iliyoboreshwa ambayo itaanza kutolewa kwa gharama nafuu kwa familia na mtu mmoja mmoja ili wapate huduma za matibabu wakati wowote.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa EFG, Jane Magigita, alisema kupitia mradi wa kuzuia na kupinga matusi kwa wanawake masokoni, wamefanikiwa kuwapa elimu ya kujitambua na kuwania nafasi za uongozi masokoni.

Alisema kampeni hiyo iliyokuwa na kauli mbiu inayosema ‘Mpe Riziki si Matusi’, imesaidia kupunguza matusi kwa wanawake kwenye masoko na kutambua haki zao wawapo kwenye majukumu ya kazi.

Kampeni hiyo ilizinduliwa jijini Dar es Salaam Februari 27, 2015 na  aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Pindi Chana, na hadi sasa imewezesha kuwafikia wanawake katika masoko ya jiji hilo.

Habari Kubwa