Makinda kuwatunuku wahitimu 309 HKMU

06Dec 2021
Joseph Mwendapole
Nipashe
Makinda kuwatunuku wahitimu 309 HKMU

MKUU wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Spika Mstaafu Anne Makinda, anatarajiwa kuwatunuku wahitimu 309 wa fani mbalimbali wakiwemo Madaktari na Wauguzi.

MKUU wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Hubert Kairuki (HKMU), Spika Mstaafu Anne Makinda.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Charles Mgone, amesema leo kuwa miongoni mwa wahitimu hao wapo madaktari 171, wahitimu 84 wa Diploma ya Uuguzi, wahitimu 43 wa Shahada ya Uuguzi  na madaktari bingwa 7 wa watoto.

Ametaja wengine wanaotarajiwa kuhitimu mwishoni mwa wiki hii kwenye chuo hicho kuwa ni mhitimu mmoja wa Shahada ya Uzamili ya Ustawi wa Jamii na wahitimu watatu wa Shahada ya Uzamili wa Afya ya Jamii.

Amesema kwa mwaka huu wa masomo chuo hicho kimefanikiwa kusajili wanafunzi 237 wa fani ya udaktari, wanafunzi 59 Shahada ya Uuguzi, wanafunzi 9 wa Shahada ya Ustawi wa Jamii na madaktari bingwa 7 wa afya ya kinamama.

Profesa Mgone amesema wamedahili pia wanafunzi madaktari bingwa 14 wa fani mbalimbali.

Katika hatua nyingine, Profesa Mgone amesema tayari HKMU imeshaanza ujenzi wa kampasi ya Boko ili kukiwezesha chuo hicho kuchukua idadi kubwa ya wanafunzi wa fani mbalimbali.

Amesema HKMU iliamua kujipanua baada ya kuona idadi ya wanafunzi inaongezeka mwaka hadi mwaka na uhitaji wa wananchi kwenye wataalamu wa sekta ya afya unaozidi kuongezeka.

Amesema katika mpango wake wa miaka mitano HKMU imeanza kuwekeza kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kukiwezesha chuo hicho kufundisha kwa njia ya mtandao.

“Wakati wa janga la corona tulifundisha kwa njia ya mtandao na sasa tunataka kuimarisha mifumo yetu kuhakikisha tunachanganya, tunafundisha mafunzo ya ana kwa ana na yale ya mtandaoni na tunataka hata shughuli zingine za kiutawala zifanyine online,” amesema

Naye Mratibu wa kongamano la waliowahi kusoma kwenye chuo hicho, Dk. Leonard Malasa, amesema kabla ya mahafali hayo  kutakuwa na kongamano la kitaaluma kwa waliowahi kusoma kwenye chuo hicho.

Amesema kongamano kubwa litafanyika siku moja kabla ya mahafali ya HKMU (ijumaa tarehe 10/12/2021) litajumuisha wanataaluma mbalimbali waliosoma hapa Kairuki na kutakuwa na wageni waalikwa mbalimbali.

“Tutajadili mambo mbalimbali tutakuwa na mada mbalimbali ambazo zitatolewa za tafiti mbalimbali ambazo wanataaluma wamefanya na miradi mbalimbali hapa chuoni siku hiyo,” amesema

Habari Kubwa