Makonda kusajili ndoa kunusuru wanawake kutapeliwa kimapenzi

13Aug 2019
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Makonda kusajili ndoa kunusuru wanawake kutapeliwa kimapenzi

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amesema amejipanga kukutana na wanawake wote wa mkoa huo, walioumizwa kwa kuahidiwa kuolewa na kisha wanaume kuingia mitini.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya Mkutano wa Viongozi Wakuu wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Makonda amesema amepanga kuzisajiri ndoa zote za mkoa huo kwa ajili ya kukabiliana na wanaume wanaowalaghai wanawake kimapenzi na kuanzisha kanzi data ya ndoa zote zilizopo kwenye mkoa wake ili kupunguza utapeli huo.

Alisema amepokea malalamiko mengi kutoka kwa wakina dada wa mkoa wa Dar es Salaam waliochoka kuumizwa na wanaume ambao wamekuwa wakiwaahidi kuwaoa na badala yake kuingia mitini.

"Nimepokea malalamiko mengi sana kutoka kwa wakinadada wa mkoa wa Dar es Salaam wengi wamechoka kutapeliwa vijana na wanaume wamekuwa wakiwaahidi kuwaoa alafu wanaingia mitini, jambo hili linafedhehesha kidogo na limefanya watoto wa kike wengi wamekuwa na majeraha moyoni," amesema Makonda

Ameongeza kuwa anataka kutumia mkutano wa SADC kuangalia nchi washiriki wa mkutano huo wanafanyaje kukabiliana na changamoto hiyo kwani kwa Tanzania ipo sheria inayosimamia haki ya mwanamke aliyeahidiwa kuolewa na kutapeliwa.

"Uzoefu tutakaoupata tunataka tuutumie na tunaompango mzuri wa kukutana na wadada wote walioumizwa.. uwezi kuwa kiongozi unaongoza watu alafu wana majeraha kwenye mioyo yao," Alisema Makonda

Wakuu takribani 16 wa nchi wanachama wa SADC, wanakutana hapa nchini kwenye mkutano wa 39 wa SADC, ambapo Rais Magufuli atakabidhiwa rasmi kijiti cha Uenyekiti wa SADC Agosti 17 kwa kipindi cha mwaka mmoja ujao.

Imeandikwa na Juster Prudence na Rahma Kisilwa na Adelina Charles, TUDARCO

Habari Kubwa