Makonda aagiza madereva mwendokasi kukamatwa

12Oct 2018
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Makonda aagiza madereva mwendokasi kukamatwa

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata madereva wa mabasi yaendayo haraka maarufu mwendokasi, ambao wanaegesha magari bila sababu za msingi na kusababisha usumbufu kwa abiria.

Aidha, Makonda amewaruhusu wananchi kuwapiga picha watoa huduma wanaowanyanyasa katika vituo vyote vya mabasi hayo ili wabainike na kuchukuliwa hatua.

Makonda alitoa maagizo hayo jana alipotembelea na kukutana na abiria wa mabasi hayo eneo la Kimara, jijini Dar es Salaam ambao walimweleza changamoto zinazowakabili.

Miongoni mwa changamoto zilizotajwa ni uchache wa mabasi, msongamano wa watu unaoweza kusababisha kuenea kwa magonjwa na kukosekana kwa usawa kwa makundi maalumu kama ya wazee, wenye ulemavu na wajawazito, wizi, misururu mirefu wakati wa kukata tiketi na baadhi ya magari kuacha abiria vituoni.

Hata hivyo, Makonda alimpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleiman Jafo, kwa kuchukua hatua za haraka na kuagiza watendaji kumaliza changamoto zinazokabili usafiri huo.

Nipashe lilishuhudia katika baadhi ya vituo vya mabasi hayo abiria wakipata huduma kama kawaida ingawa wakilalamikia uchache wa mabasi.

Juzi abiria wanaotumia usafiri wa mabasi hayo walikumbana na changamoto ya kukaa kwenye vituo vya mabasi kwa zaidi ya saa mbili wakisubiri usafiri huo kutokana na baadhi ya madereva kugoma.

Hali hiyo ilisababisha vurugu katika kituo cha Kimara na usumbufu mkubwa baada ya abiria kuvunja utaratibu na kuingia kwenye barabara kushinikiza kupanda.

Kufuatia kuzuka kwa vurugu hizo, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya mradi huo, Deus Bugaywa, alitoa taarifa inayoeleza kuwa, matatizo ya usafiri yaliyoibuka yalisababishwa na hujuma.

Alidai kuwa, madereva wawili waliokuwa wanatoa mabasi nje ya karakana hiyo kwa ajili ya kuanza kutoa huduma waliyaegesha kwenye milango miwili ya kutokea kuziba mengine yasitoke huku wakiondoka na funguo na kwenda kusikojulika.

Alisema hali hiyo ilisababisha mabasi kuchelewa kutoka na kuleta usumbufu mkubwa kwa abiria waliokuwa vituoni wakisubiri huduma.

Kwa upande, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi), Seleman Jafo, alilazimika kumwagiza Naibu Waziri wake Joseph Kakunda, kufanya kikao kitakachojumuisha Mtendaji Mkuu wa Dart pamoja na mtoa huduma Udart ili kubaini matatizo makubwa ambayo yamekuwa yakisababisha mradi huo kudorora.

Pia alimwagiza Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mussa Iyombe, kufanya uchunguzi katika ofisi ya Dart kuona kama wapo watendaji wanaokwamisha huduma hiyo na kuwaondoa mara moja.

Habari Kubwa