Makonda akabidhi ofisi na kuomba msamaha

04Aug 2020
Joseph Mwendapole
Dar es Salaam
Nipashe
Makonda akabidhi ofisi na kuomba msamaha

ALIYEKUWA Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amekabidhi ofisi kwa Mkuu wa Mkoa mpya, Aboubakary Kunenge na kuwaomba msamaha wakazi wake huku akiwataka wamwache akapumzike kwa amani na kumlea mtoto wake.

Hafla ya makabidhiano ilipangwa kufanyika saa 3:00 asubuhi lakini Makonda aliingia kwenye ofisi hiyo saa 5:15 na kulakiwa na kundi kubwa la wapigapicha na waandishi wa habari.

Waandishi hao ambao walifika mapema kwenye ofisi hiyo majira ya saa 2:30 asubuhi, walianza kumpiga picha tangu anashuka kwenye gari lake nje ya ofisi hizo hadi anaingia ofisini.

Baada ya kuingia, waandishi wa habari waliarifiwa na maofisa wa ofisi hiyo kuwa Makonda ana mazungumzo na Mkuu wa Mkoa yatakayochukua dakika 20 na ndipo wataruhusiwa kuingia.

Alipoanza kuzungumza, Makonda alisema hatasahau vita vitatu ambavyo alipigana na kusababisha watu kupiga kelele ikiwamo ya kupambana na mapapa wauzaji na wateja wa dawa za kulevya.

Makonda alisema anawapenda wakazi wa Dar es Salaam kwa kuwa amewatumikia kwa uaminifu na siku zote alikuwa akimwomba Mungu amsaidie asifanye baya ambalo ataulizwa mbinguni.

“Ninaamini nimetumia uwezo wangu wote akili zangu zote na vipaji vyangu vyote hatimaye naamini mwendo nimeumaliza salama. Kama binadamu inawezekana nina mapungufu (upungufu) yangu mnisamehe pale nilipoenda kinyume cha mapenzi yenu,” alisema.

Makonda alisema Julai 15, aliamua mwenyewe kuondoka na kwenda kwenye majukumu mengine baada ya kuacha alama kwa wakazi wa Dar es Salaam kwa kazi kubwa aliyofanya.

Alisema pamoja na kelele za watu, Rais John Magufuli aliendelea kumwamini na kumpa moyo hali iliyosababisha kuendelea kupambana na watu hao na hatimaye kushinda mapambano.

Pia alisema atamuenzi Rais Magufuli kwa vitendo kwa kuwa ni mtu wa mfano kwake na atakayejaribu kumsema vibaya, atasimama kupambana naye hata kama hayuko kwenye nafasi yoyote.

Makonda aliwashukuru waliokuwa wasaidizi wake wakiwamo wafagizi ambao alisema wasingekuwa wema wangeweza hata kutumiwa na watu wabaya kumwekea sumu kutokana na watu aliokuwa akipambana nao.

“Nawashukuru wote tuliofanya kazi pamoja kwa sababu vita nilizopambana ningeweza kupewa sumu lakini wamekuwa waaminifu na nimeondoka ofisini nikiwa na furaha,”

Alisema anamshukuru mke wake kwa kuwa mvumilivu kwa maneno ya kashfa na kejeli dhidi yake kwa miaka yote ya utumishi wake kwenye nafasi hiyo na kwamba ataendelea kusimamia imani yake bila kujali maneno ya ovyo anayohusishwa nayo.

“Mke wangu aliniambia kuwa mbona kuna maneno mengi huku instagram kuhusu wewe nilidhani watu watakuacha baada ya kuacha kazi mbona wanakufuatilia nikamwabia waache waseme ukiona husemwi jua huna la maana. Nilimwambia kusema kwangu ndio mtaji wangu na huwezi kusemwa kama huna la maana,” alisema Makonda

Makonda alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua Kunenge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwani ni mchapakazi ambaye atayaendeleza yale yote mazuri waliyokuwa wakiyafanya pamoja.

Hata hivyo, alimtaka mkuu mpya wa mkoa kutosikiliza majungu akidai kuwa asilimia 70 ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam ni wambea na wachonganishi

Habari Kubwa