Makonda amwaga machozi kanisani

06Mar 2017
Frank Monyo
Dar es Salaam
Nipashe
Makonda amwaga machozi kanisani
  • Ni katika ibada ya maombezi ya vyeti na mikataba ya ajira kwa waumini ...

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda jana alimwaga machozi mbele ya waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Kimara wakati wa ibada ya Jumapili.

Mkuu huyo wa Mkoa ambaye alikuwa ni mmoja wa watu waliohudhuria ibada ya siku hiyo, alijikuta akibubujikwa na machozi baada ya kupewa nafasi ya kuwasalimia waumini wa kanisa hilo.

Kabla ya kuanza kulia, Makonda alikuwa ametumia muda wake madhabahuni kueleza nia yake ya kuendelea na mapambano ya dawa za kulevya jijini.

Misa ya jana katika Usharika wa Kimara ilikuwa ni mahsusi kwa ajili ya kuombea vyeti vya kuzaliwa, vya masomo na mikataba ya ajira kwa Wakristo wa hapo.

Wakati wa akitoa salamu hizo, Makonda alisema nchi kupitia Dar es Salaam imekuwa ndiyo mlango wa kuingiza na kutoa dawa za kulevya hivyo hatoweza kukaa kimya na kushuhudia watoto na taifa vikiangamia.

Alisema Dar es Salaam ndiyo lango kubwa la uchumi wa nchini kwa kuchangia asilimia 17 katika pato la taifa huku asilimia 80 ya mapato yanayokusanywa na TRA yanatoka mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema, lakini watu wameamua kutumia lango hilo kuangamiza vijana kwa kupitisha dawa za kulevya.
“Sitakaa kimya wala sitaruhusu uovu ukatize katika anga ya utawala niliyopewa," alisema Makonda.

Alisisitiza kuwa hatoacha kupigana vita hivyo akiwa hai, hasa kwa sababu amepewa bendera ya Tanzania yenye kuashiria mamlaka.
Alisema atasimama hadi tone la mwisho la damu yake kuhakikisha "jina la Yesu linainuliwa".

Alisema watu hawapaswi kulalamika wala kuhuzunika kwa watu ambao wanaongea kila siku kwenye mitandao ya kijamii, kwani hiyo ni ishara kuwa kazi inayofanyika katika ulimwengu wa roho inalipa na inaonekana na inalipa.

Vita dhidi ya dawa za kulevya nchini imepata msukumo mpya tangu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ataje orodha ya watu 65 ambao alitaka waisaidie polisi kuhusu biashara ya madawa ya mwanzoni mwa mwezi uliopita.

Kabla ya kutaja orodha hiyo iliyokuwa na askofu Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, wafanyabiashara na wanasiasa, Makonda alikuwa ametoa orodha ya Polisi 12 na wasanii ambao walitakiwa pia kufika Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano.

Katika awamu ya tatu ya vita mpya dhidi ya biashara ya mihadarati ya Makonda, mkuu huyo wa mkoa alikabidhi orodha ya watu 97 wanaodaiwa kujihusisha na dawa za kulevya kwa Kamishna Mkuu mpya wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Rogers Sianga.

SIYO RAIA
“Hakuna mcha Mungu atakayeacha kusimama katika hili ambalo Rais wetu (John Magufuli) ametuagiza na kutuelekeza," alisema Makonda, "na kuendelea kupiga kelele hizi ndogo ndogo."

"Hivi sasa wameenda mbali zaidi na kudai kuwa mke wangu siyo raia wa Tanzania... kila kukicha wanatafuta jambo jipya.”

Kwa mujibu wa askofu Gwajima, jina halisi la mkuu huyo wa mkoa ni Daudi Albert Bashite na pia amesoma kwa kutumia vyeti vya watu wengine baada ya kupata daraja sifuri Kidato cha Nne.

Makonda jana alisema pamoja na kuwapo na sababu nyingi za yeye kuwapo hapo, lipo jambo ambalo alikuwa akifikiria kulisema mbele ya madhabau hiyo endapo angepata nafasi.

“Najua kazi ya waumini wa kanisa hili si bure mbele ya Bwana (Mungu) na ni wazi kuwa tunapita katika kipindi cha kuidhalilisha kazi ya msalaba kwakuwa kipindi hiki kinamtaka kila mcha Mungu katika mkoa wetu kukaa sawa na Mungu wake," alisema Makonda.

"Uongozi wa kweli unaanza kwenye familia na familia ikikaa vizuri mtaa utakaa vizuri, kata itakaa vizuri, wilaya, mkoa na hatimaye taifa litapeperusha bendera yenye sifa nzuri.”

Habari Kubwa