Makonda atangaza rasmi kumuenzi Askofu Pengo

27Jan 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Makonda atangaza rasmi kumuenzi Askofu Pengo

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameahidi kutoa barabara moja ya lami itajayopewa jina la Askofu Mkuu wa Kanisa katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kwa ajili ya kuenzi busara zake, utumishi na msimamo wake wa kuwaleta watu pamoja.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda

Makonda alitoa ahadi hiyo jana wakati akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa majengo ya Shule ya Sekondari St. Joseph Millennium, iliyoko Goba nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

 

Alisema atatoa barabara moja kati ya mpya tano zinazojengwa katika jiji hilo, ipewe jina la Pengo ikiwa ni heshima ya kukumbuka mema anayotenda.

 

“Askofu Pengo ni kiongozi wa mfano wa kutunza amani yetu, hivyo ni vyema kuangalia namna kuanza kuuenzi utumishi wako katika mkoa wetu na taifa kwa ujumla. Mkoa tutatoa barabara ambayo tutaiita jina lako kwa sababu unastahili heshima inayohitajika kukumbukwa na vizazi vijavyo,” alisema Makonda.

 

Alisema sababu nyingene ya kumtunuku barabara kiongozi huyo wa kiroho ni kutokana na kutoa kauli za msimamo zinazowaleta watu pamoja badala ya kuwagawanya.

 

Makonda alisema ndani ya mwezi mmoja atawasilisha taarifa ya utekelezaji wa ahadi hiyo ofisini kwake.

 

Kwa upande wake Kardinali Pengo alisema lengo la kupatiwa barabara hiyo liwe kwa ajili ya kuwaombea wanaoitumia ili kusiwe na wahuni na wadokozi.

 

“Naamini hamtanihesabia na makosa yatakayofanyika kwenye barabara hiyo, maana mnaweza mkanipa ile iliyo karibu na St. Joseph mkiamini ni nzuri lakini kila siku nasikia mayowe,” alisema.

 

Sambamba na hilo, Makonda alizipongeza shule za seminari kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne kwa sababu ya kuzingatia maadilini na kutofanya udanganyifu.

Katikac hatua nyingine, aliwatahadharisha wanasiasa walioko katika mkoa wake wenye tabia za kuwakebehi na kuwatukana viongozi wa dini kuacha na endapo wataendelea atawachukulia hatua.

 

Aidha, aliwaagiza maofisa elimu sekondari na msingi kusimamia utekelezaji wa somo la dini katika shule zote za mkoa hilo kwa lengo la kuwafundisha maadili na kuwa na taifa lenye maadili.

 

Awali Mkuu wa shule hiyo, Sister Caroline Kokutekana, alisema matokeo ya kidato cha nne mwaka jana kati ya wanafunzi 111 waliofanya mitihani ya kidato cha nne, 62 walipata daraja la kwanza, 45 walipata daraja la pili na wanne walipata daraja la tatu.

 

Alisema pia matokeo ya kidato cha pili kati ya wanafunzi 142 kati yao 139 walipata daraja la kwanza, watatu daraja la pili.

 

Akizungumzia majengo yaliyozinduliwa jana alisema ni mabweni kwa ajili ya wanafunzi ambayo pia yamefungwa vifaa vya kisasa vya kutambua harufu ya moshi na rangi yenye harufu kali ili kujikinga na majanga mbalimbali.

00000

 

Na Ibrahim Yassin, MBEYA

WAHUDUMU wa baa na nyumba ya kulala wageni iitwayo Malema Lodge iliyopo mtaa wa Sinde jijini Mbeya,waliolazwa hospitalini baada ya kunyweshwa vinywaji na soda zinazodaiwa kuwa na dawa za kulevya na watu wasiofahamika usiku wa kuamkia juzi wametolewa hospitalini hali zao zikiimalika.

Akizungumza leo (jana) kwa njia ya simu,mmiliki wa Lodge hiyo,Merry Malema,alisema vijana wake baada ya kutoka hospitali na kuangalia vipimo vya kitabibu imebainika walilazwa baada ya kuzidiwa na kiwango cha dawa walizolishwa lakini hawakubakwa.

Malema ambaye pia ni diwani wa viti maalum (CCM) alisema taarifa iliyotolewa na baadhi ya watu kuwa vijana wake walibakwa siyo sahihi kwani wakati vijana hao wamekumbwa na tukio hilo,hakuna mtu ama shuhuda aliyeweza kuona na kwamba kilichofanyka kwa watu hao ni kupora fedha za mauzo ya siku nzima.

‘’Ndugu mwanahabari leo polisi watano walifika nyumbani kwangu,kuwaona vijana wangu ambao wanaendelea vizuri,wakiwa na fomu za majibu wa madaktari zikionyeshwa vijana wake hawakubakwa zaidi ya kula vyakula vya sumu’’alisema.

Aliongeza kuwa baada ya taarifa kutolewa ndugu wa vijana hao waliopo nje ya wilaya ya Mbeya walifika kuwaona huku wakisema wamesikia taarifa kuwa ndugu zao walifanyiwa unyama huo na walipowaona wakiwa vizuri walifarijika.

Alisema wakati watu hao watatu wanaingia usiku wa saa tano katika baa hiyo,kumbe kuna mwenzao alipanga katika gesti hiyo alikaa siku mbili ndipo waliposhirikiana kutimiza azma hiyo kwa kuchukua fedha zote za mauzo ya nzima upande wa baa na gesti.

Tukio hilo la uvamizi huo,ulifanyika juzi usiku wa saa tano,ambapo watu watatu waliingia ndani ya baa na kuanza kutoa ofa ya vinywaji na biskuti wakati geti limefungwa ndipo wakampa pia mlinzi soda na biskuti na baada ya muda mfupi walizidiwa na watu hao kutekeleza hazma yao ya uporaji na taarifa zimeeleza kuwa hawakubakwa.

 

 

 

 

 

 

 

Habari Kubwa