Makonda, awataka vijana kuwa wabunifu

18Mar 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Makonda, awataka vijana kuwa wabunifu

MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amewataka vijana kuwa wabunifu na kupambana kwa ajili ya kufikia  malengo yao badala ya kusubiri kusaidiwa.

Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Mhe. Paul Makonda (katikati) na Meneja wa QNET, kanda kusini ya Afrika Biram Fall (kushoto) wakikata utepe kuzindua rasmi maonesho ya bidhaa za QNET 2019 jijini humo. Kulia ni Mshauri wa Biashara wa QNET Tanzania, Edward MkonyI.

Makonda alitoa wito huo juzi wakati akizundua maonyesho ya bidhaa na huduma za kampuni ya mauzo ya moja kwa moja QNET jijini Dar es salaam.

Makonda alijitolea mfano kuwa, alipambana mwenyewe tangu akiwa mdogo ili kupata elimu bila kutegemea wazazi wake ambao hawakuwa na elimu.

“Vijana tuache kusubiri kusaidiwa tukiwa tumekaa. Mimi nimezaliwa familia ya baba ambaye hajasoma hata darasa moja kwa sababu siku ya kwenda kuandikishwa shule aliambiwa darasa limejaa, mama yeye alisoma hadi darasa la saba hivyo sikuwa na msaada wowote wa kupata elimu lakini nilipambana kupata elimu hadi hapa nilipofika ," alisema Makonda.

Aliongeza kuwa, “Kunzishwa kwa kampuni hii ya QNET tunaona ni juhudi za vijana ambao waliamua kukaa na kubuni na leo wanafanya biashara dunia nzima baada ya kunzia Asia leo ipo Tanzania ni jambo la kujifunza kwa vijana."

Makonda alisema maisha yake ni mfano wa kufanya kazi kwa bidii na kujiamini katika kitu chochote na njia pekee ya kuleta mabadiliko na maendeleo kwa mtu binafsi familia na jamii kwa ujumla.

Kwa upande wake Meneja Mkuu wa QNET,  Kanda ya Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika, Biram Fall, alisema maonyesho hayo yenye jina lenye maana ya Kuishi Kikamilifu, yanafanyika kila mwaka katika nchi mbalimbali duniani kwa lengo la kuonyesha bidhaa zake na huduma kwenye masoko mapya.

"Tunatoa aina mbalimbali za bidhaa za kiwango cha juu na huduma kwa wateja wetu kuwasaidia waweze kuishi maisha yenye uwiano sahihi, na pia kutatua tatizo la msingi kama vile elimu, ufahamu, na maendeleo binafsi kupitia program za mafunzo yetu, ambayo yanawasaidia katika safari yao ya kujiajiri mwenyewe," alisema.

Alisema zaidi ya watu 2,000 walipata fursa ya kuona bidhaa za mfano katika maonyesho hayo na kufundishwa namna ya matumizi ya bidhaa na faida zake kwa wateja na watumiaji wa mwisho.  

Pia wananchi walipata fursa kujifunza mbinu mbalimbali za kibiashara kutoka kwa wataalamu wa bidhaa na biashara walikuwepo kwa ajili ya kujibu swali kuhusu ulimwengu wa QNET.

Maonyesho ya Dar es Salaam yalitanguliwa na mfululizo wa maonyesho kama hayo yaliyofanikiwa nchini Togo, Guinea, Ivory Coast, Senegali, Burkina Faso na Cameroon mwaka jana.

Habari Kubwa