Makonda kuwatimua wamachinga wasio na vitambulisho

01Jun 2019
Mary Geofrey
DAR
Nipashe
Makonda kuwatimua wamachinga wasio na vitambulisho

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesisitiza msimamo wa kuwatimua wafanyabiashara wadogo maarufu ‘wamachinga’ ambao hawana vitambulisho na hana mpango wa kuwaongezea muda.

wamachinga.

Juzi Makonda, alisema Jumatatu ijayo itakuwa mwisho kwa wafanyabiashara wadogo kuendelea kufanyabiashara katika jiji hilo kama hawana vitambulisho.

Akizungumza na Nipashe jana, Makonda alisema hana mpango wa kuongeza muda kwa wafanyabiashara hao kwa sababu walishatoa muda wa miezi sita kuwabembeleza kuvichukua.

“Kuanzia Jumatatu hatutaki kuona ‘Mmachinga’ ambaye atakuwa anauza au kutembeza bidhaa zake katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam, bila kuwa na kitambulisho cha kufanya biashara,” alisema Makonda.

Alisema msimamo wa mkoa huo ni wafanyabiashara wote kuwa na vitambulisho ili kuwatambua na kufanyabiashara kwa uhuru katika maeneo yao.

Aidha, alisema watawakamata wafanyabiashara watakaokaidi agizo hilo na watakaokamatwa watachukuliwa hatua za kisheria.

“Kama wewe ni mhalifu na ukakamatwa unachukuliwa hatua, tumeshatoa muda wa miezi sita kwa wafanyabiashara kuchukua vitambulisho, siamini kama wapo ambao wataendelea kufanyabiashara katika mkoa huu bila kutambulisho tena,” alisema Makonda.

Juzi Makonda aliwaeleza waandishi wa habari kuwa, alipita katika mitaa zaidi ya tisa ya jiji hilo na kukuta baadhi ya wafanyabiashara wakiwa hawana vitambulisho hivyo.

Alisema wafanyabiashara ambao hawana vitambulisho hivyo wafike ofisi za wilaya na kata kwa ajili ya kupatiwa.

Makonda alisema Rais John Magufuli, aliukabidhi mkoa huo vitambulisho 175,000 akiamini kuwa vitamalizika kulingana na wingi wa wafanyabiashara katika jiji hilo.

Desemba 10, mwaka jana, Rais Magufuli alitoa vitambulisho 670,000 kuwatambua wafanyabiashara wadogo nchini kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa.

Kwa upande wa wafanyabiashara katika soko la Kariakoo, walilalamika kupoteza vitambulisho hivyo na kumuomba Makonda kuongeza muda ili kufuatilia suala hilo.

“Mimi nilishachukua kitambulisho ila kimepotea, kama Makonda angetuongezea muda tukaanza kufuatilia tena kwa waliotupatia ili watupe kibali cha kutambulika kwa sababu hatuna tena fedha za kununua vitambulisho vingine tena,” alisema Zuber Mkinga, muuza viatu katika soko hilo.

Rais Magufuli alitoa vitambulisho hivyo katika mkutano wake na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), wakuu wa mikoa yote nchini, uliokuwa ukijadili namna ya kuboresha mazingira ya ukusanyaji mapato.

Alisema kwa muda mrefu amekuwa akiiagiza TRA pamoja na halmashauri kutowatoza kodi wajasiriamali wadogo ambao mitaji yao haizidi Sh. milioni nne, lakini utekelezaji wake umekuwa wa kusuasua.

Kila mkoa ulipewa vitambulisho 25,000 na kila mjasiriamali mdogo atalipia Sh. 20,000 kupata kitambulisho hicho na fedha hiyo kupelekwa TRA.

Kwa malipo hayo, kila Mkuu wa Mkoa atakusanya Sh. milioni 500 na ikibidi aagize vitambulisho vingine kwa ajili ya watakaovihitaji.

Habari Kubwa