Makonda: Lowassa tutamkumbuka kwa mambo mengi amekuwa kiongozi mwema

11Feb 2024
Beatrice Shayo
Nipashe Jumapili
Makonda: Lowassa tutamkumbuka kwa mambo mengi amekuwa kiongozi mwema

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimetuma salamu za rambirambi kwa familia ya aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na atakumbukwa kwa mambo mengi amekuwa kiongozi mwema kwa nafasi zote alizozishika.

Hayo yalisemwa jana mkoani Ruvuma na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda, wakati akizungumza na wananchi wa mkoa huo ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya mikoa 20.

“Niungane na Mwenyekiti wetu wa chama na Rais Samia Suluhu Hassan, kutoa pole kwa niaba ya chama chetu kwa familia ya mzee wetu Lowassa kwa kuondokewa na mpendwa, kiongozi wetu na mwanachama wetu ambaye amefariki leo majira ya saa nane mchana,”alisema Makonda.

Makonda amesema kwa niaba ya CCM wanatoa pole kwa wanachama, wapenzi wa chama, wakereketwa na Watanzania wote kwa ujumla amekuwa kiongozi mwema kwa nafasi zake zote ametoa mchango kwa taifa.

Makonda amesema Hayati Lowassa atakumbukwa kwa mambo mengi kwa umahiri wake wa kujenga hoja kwa nyakati tofauti wamekubaliana na maamuzi ya mwenyezi Mungu.

Amesema Rais Samia ametangaza maombolezo na kushushwa kwa bendera nusu mlingoti kwa siku tano.