Makonda: Ruksa bodaboda, bajaji kuingia katikati jiji Dar

02Apr 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Makonda: Ruksa bodaboda, bajaji kuingia katikati jiji Dar

MKUU wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameruhusu pikipiki za miguu mitatu maarufu kama bodaboda na bajaji kupeleka abiria katikati ya jiji mpaka hapo ugonjwa wa Ccrona utakapodhibitiwa nchini.

Pia amewaomba wenye nyumba na maeneo ya biashara kupunguza bei ya kodi kwa asilimia 50 kwa kipindi cha miezi mitatu, ili kuwawezesha wananchi kumudu gharama za maisha na kulipa.

Makonda alitoa kauli hiyo jana alipofanya ziara katika stendi ya daladala ya Makumbusho, Kinondoni jijini humo.

Alisema katika kipindi hiki ambacho nchi inachukua tahadhari ya kupambana na ugonjwa huo ni vyema bodaboda zikasaidia kubeba abiria kupeleka katikati ya jiji huku akiwasisitiza madereva kuzingatia sheria.

“Masharti yaliyopo ni ya siku zote kwamba bodaboda ni lazima mzingatie sheria, ikiwa ni pamoja na kuvaa helmeti, na kutokuingia kwenye barabara ya Mwendokasi. Lakini zaidi ya yote mna ruhusa ya kuingia katikati ya jiji na kuwabeba abiria wenye uwezo wa kupanda usafiri wao binafsi na kuhakikisha wanawahi kazini,” alisema Makonda.

MWENDOKASI

Kuhusu usafiri wa magari yaendayo kwa haraka, Makonda alisema usafiri huo hauko katika mamlaka yake, lakini ameandika barua kupeleka Ofisi ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ili iingilie kati na kuruhusu magari 200 ambayo hayafanyi kazi kutokana na mgogoro uliopo.

“Suala la mwendokasi haliko chini ya mamlaka yangu, iko Tamisemi, lakini hivi tunavyozungumza watu wangu wanamalizia kuandika barua, nimemuomba waziri aingilie kati, ninafahamu yako mabasi si chini ya 200 ya mwendokasi yamepaki Ubungo, Bandari kavu.”

“Nafahamu yale magari kuna mgogoro, lakini kutokana na hali tuliyonayo sasa hivi, nimemwandikia barua ya kumuomba aone uwezekano wa kuyaruhusu yale magari yaingie kwenye laini ya mwendokasi kutoka Kimara ili wananchi wasirundikane na kubanana, waingie mjini na kuchapa kazi huku wakilinda afya zao.”

KODI WENYE NYUMBA

Makonda alisema kutokana na kuyumba kwa biashara nyingi kwa sababu ya ugonjwa huo, ni vyema wamiliki wa nyumba za biashara na nyumba za kupangisha kwaajili ya makazi kodi ikapunguzwa kwa asilimia 50 kwa kipindi cha miezi mitatu.

“Kutokana na changamoto ya ugonjwa huu wa corona, baadhi ya biashara haziendi vizuri, lakini wako watu ambao wamepanga kuanzia wanaoishi kwenye chumba kimoja, vyumba viwili, wako waliopanga kwenye ofisi au apartment,”alisema Makonda na kuongeza:

“Nimeanza kuzungumza na wamiliki wa majengo baadhi yao wamekubali, naomba kutoa rai hii kwa wenye nyumba, wenye majengo, yawe ni ofisi, ‘apartment’ au majumba ya kawaida au ni vyumba vya vibanda. Naomba kwa kipindi hiki cha miezi mitatu, mpunguze kodi kwa asilimia 50, kuwawezesha wananchi wamudu hali ya kawaida.”

“Wananchi hawa wana changamoto ya biashara zao, biashara ya nyumba ni matokeo ya biashara inayopatikana kutokana na mtu kufanya kazi yake. Kama anaenda na ana changamoto yake huko ofisini, biashara haina wateja, tena unakuja kumuua kwenye kodi yako kudai pale pale, ninawaombeni wenye nyumba na wenye majengo wote mkubali.”

Makonda alisema tayari amezungumza na wenye majengo na nyumba 50 na wamekubali kushusha kodi kwa kutoza nusu ili kumsaidia mpangaji apate akiba ya kununua chakula cha kutunza ndani hususani katika kipindi hiki.

“Siyo kwamba natangaza bei mpya ya upangaji, isipokuwa nimeomba kama ombi kwa sababu jukumu langu pia ni kusemea mwananchi wa hali ya chini ambaye hana uwezo wa kujisemea,” alisema Makonda.

WATU WABAKI NYUMBANI

Alisema katika kipindi hiki cha mlipuko wa ugonjwa ni vyema wasio na shughuli za kufanya mjini wakabaki nyumbani badala ya kuzurura kwenda katikati ya mji bila shughuli yoyote ya maana.

“Kama huna ulazima wa kwenda baa, kama unapenda muziki, unapenda disko, unataka kucheza, fungua nyumbani kwako, weka muziki, cheza na mkeo. Ni bora ukawa na afya njema kuliko ukaugua ugonjwa wa corona.”

UPOKEAJI WAGENI UWANJA WA NDEGE

Aliwaomba wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuacha kwenda kuwapokea wageni wao wanaoingia katika uwanja wa ndege kutoka nje ya nchi na kwamba serikali kupitia watu walioandaliwa ndio wanajukumu la kuwapokea na kuwahifadhi kwa siku 14 kama maelekezo yalivyotolewa.

Aliwataka wakazi wasio na ulazima wa kutoka au kuingia Dar es Salaam wabaki katika mikoa yao.

HELIKOPTA KUPULIZA DAWA

Makonda alisema anaendelea kuchukua jitihada za kila namna kuhakikisha anawalinda wananchi wa mkoa huo ikiwamo kupulizia dawa.

“Mungu akipenda tunategemea kwamba kutakuwa na helikopta za kupulizia dawa katika Jiji la Dar es Salaam, kuhakikisha tunaua wadudu wote, tumeanza na mashine ya kupulizia, tunatumia gari zote za zimamoto na gari za polisi,” alisema Makonda.

Habari Kubwa