Makumbusho ya kisasa ya sokwe mtu kujengwa

25Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
ARUSHA
Nipashe
Makumbusho ya kisasa ya sokwe mtu kujengwa

TAASISI ya Kimataifa ya Jane Goodall, imeanza ujenzi wa makumbusho maalum ya sokwe mtu jijini Arusha yatakayokuwa na teknolojia ya kisasa zaidi inayoendana na ulimwengu, yakiwa ya kwanza kujengwa duniani.

sokwe mtu.picha:bbc

Akizungumza wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi huo jana, mwasisi na mwenyekiti wa taasisi hiyo, Dk. Jane Goodall, alisema kujengwa kwa makumbusho haya jijini hapa ni kutokana na muhimu wake kwa Watanzania na wageni wa kimataifa watakaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini.

Dk. Jane Goodall alieleza kuwa watalii watakaotembelea vivutio mbalimbali vya utalii wakiwamo Watanzania wenyewe watatumia kituo cha makumbusho haya kupata elimu juu ya umuhimu wa masuala ya uhifadhi wa maliasili, uhifadhi wa mazingira na wanyamapori.

“Makumbusho haya hayatatumika kwa ajili ya watafiti, wanasayansi, wanafunzi pekee bali yamejengwa kwa faida ya jamii mbalimbali duniani,” alisisitiza.

Alisema kituo hicho kitatumika kuwaunganisha vijana katika kujitolea na pia kuonyesha kazi mbalimbali zinazofanywa na Taasisi mbalimbali katika suala zima la uhifadhi.

Alifafanua kwamba amekuwa akialikwa sehemu mbalimbali duniani kuzungumza na wanafunzi na waumini katika nyumba za ibada kuhusiana na uhusiano wa moja kwa moja kati ya imani na huruma kwa viumbe wote wakiwamo wanyama na binadamu.

Kwa mujibu wa utafiti wa Dk. Goodall, sokwe anamkaribia binadamu kwa zaidi ya asilimia 90 ambapo pia utafiti wake unabainisha kwamba mahala anapolala sokwe ni bora zaidi kuliko malazi ya binadamu.

Mwenyekiti Mwenza wa taasisi hiyo, James Lembeli, alisema makumbusho hayo ni dhamana kubwa iliyotolewa na taasisi hiyo kwa Watanzania katika suala zima la uhifadhi.

“Makumbusho haya yatatoa taswira halisi juu ya dira ya masuala ya uhifadhi na umuhimu wake kwa dunia nzima ambapo pia katika makumbusho haya utapatikana utafiti uliofanywa na Dk.  Goodall na machapisho yake kwa faida ya dunia nzima,” alisema Lembeli.

Lembeli ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa kamati ya bunge ya Maliasili,Ardhi na Mazingira, alisema Dk. Jane Goodall kwa zaidi ya miaka 60 ametumia muda wake mwingi kufanya utafiti kuhusu masuala ya maisha, tabia na mwenendo wa sokwe mtu.

Alisema wakati akianza shughuli za utafiti wa sokwe katika hifadhi ya Gombe ilikuwa vigumu sana sokwe hao kumkaribia kutokana na kumwogopa mtu mweupe.

Lembeli alisisitiza umuhimu kwa vijana kutumia taasisi hiyo kuendeleza shughuli za utafiti na uhifadhi ambapo mtafiti huyo taasisi yake imetilia mkazo mipango bora ya matumizi ya ardhi.

Lembeli alisema makumbusho hayo ni ya kwanza kujengwa na taasisi hiyo duniani ambapo alisisitiza umuhimu wa Serikali ya Tanzania kutambua umuhimu wa mtafiti Dk. Jane Goodall katika suala la uhifadhi, matumizi bora ya ardhi na mchango wake katika masuala yote ya uhifadhi.

Makumbusho hayo yanatarajia kukamilika mwakani   wakati taasisi hiyo itakapokuwa ikiadhimisha miaka 60 tangu Dk. Jane Goodall aanze shughuli za utafiti wa sokwe katika Hifadhi ya Taifa Gombe.

Naye, mtafiti Anthoony Tonny wa taasisi hiyo, alisema inakadiriwa kuwa Tanzania bado ina sokwe kati ya 1,700 na 2,300 ambapo Taasisi, na kwamba taasisi hiyo  inafanya kazi na nchi zaidi ya 30 duniani.

Dkt Jane Goodall, ambaye ni Raia wa Uingereza, alianza shughuli za utafiti rasmi katika muala ya sokwe katika hifadhi ya Gombe miaka ya 1960 akiwa na umri wa miaka 26, na  hivi sasa ana umri wa miaka 86

 

Ujenzi wa makumbusho haya yatakayogharimu zaidi ya shilingi bilioni moja, unafanyika katika eneo la Cultural Heritage, baada ya mmiliki wa eneo hilo, Saifudin Khanbhai, kutoa bure sehemu ya ardhi.

Mbali na ujenzi wa makumbusho hayo, taasisi ya Jane Goodall imetoa zaidi ya shilingi bilioni 45 katika miradi mbalimbali hususan ya uhifadhi wa misitu ya asili, matumizi bora ya ardhi na uhifadhi wa sokwe.

Habari Kubwa