Makusanyo kiduchu ardhi yamchefua Naibu Waziri

25Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Sumbawanga
Nipashe
Makusanyo kiduchu ardhi yamchefua Naibu Waziri

MAKUSANYO kidogo ya kodi ya pango la ardhi katika halmashauri za Mkoa wa Rukwa, yamemkera Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, baada ya kuelezwa kuwa hadi kufikia Desemba 2019, jumla ya Sh. milioni 148.2 zilikusanywa na halmashauri zote nne, sawa na asilimia 7.9

Akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mkoa huo jana, Dk. Mabula alikutana na alikutana na watumishi wa sekta ya ardhi na kushangazwa na namna maofisa ardhi wa halmashauri hizo wasivyofuatilia makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kiasi cha kuzifanya halmashauri hizo kukusanya kiasi kidogo cha fedha.

Alisema haiwezekani ndani ya miezi sita halmashauri nne za Mkoa wa Rukwa zikusanye asilimia 7.9 ya kodi ya pango la ardhi, akisisitiza kuwa inatia shaka kama halmashauri hizo zitafikisha hata asilimia hamsini ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2019/2020.

Kwa mujibu wa taarifa ya mkoa huo iliyosomwa na Mrasimu Ramani wa Mkoa wa Rukwa, Kelvin Maungi, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020, halmashauri za mkoa huo zilikadiriwa kukusanya jumla ya Sh. bilioni 1.88.

Maungi alisema Manispaa ya Sumbawanga ilikusanya kiasi cha Sh. 94,253,273, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi Sh. 16,494,189, Kalambo Sh 1,793,550 na Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Sh. 35,680,575 na hadi hadi Desemba 2019, jumla ya Sh. 148,221,587 zilikuwa zimekusanywa kwa halmashauri zote, sawa na asilimia 7.9.

"Wakurugenzi wako 'busy' na masuala mengine, mkoa mzima una asilimia 7.9 ya makusanyo ya kodi ya pango la ardhi, ni aibu na hamuwezi kufikia asilimia 50 ya makusanyo, naagiza wote mkafanye uhakiki wa wadaiwa wa kodi ya ardhi na muwapelekee ilani ili watakaokaidi, wafikishwe kwenye mabaraza ya ardhi," aliagiza.

Naibu Waziri huyo aliagiza kufikia Machi mwaka huu, lazima kuwe na mabadiliko ya utendaji kazi kwenye sekta ya ardhi kwa halmashauri za mkoa huo, vinginevyo atafikiria kama wakuu wa idara wanatosha kuendelea na nafasi zao.

Dk. Mabula alisema mikoa yote aliyoitembelea kwenye ziara zake za kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi, imefikisha au kuvuka asilimia 30 ya makusanyo ya kodi ya ardhi, lakini Mkoa wa Rukwa umemsononesha.

Aliwamwagiza Kamishna wa Ardhi Msaidizi Kanda, Thadei Kabonge, kutoa maelezo kuhusiana na utendaji kazi wa wakuu wa idara kama wanafaa kushika nafasi zao.

Alisema taarifa zilizokuwa kwenye mfumo wa kielektroniki zinaonyesha Manispaa ya Sumbawanga ilitakiwa kukusanya Sh. bilioni 6.7, Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Sh. milioni 20, Kalambo Sh. milioni 1.6 na Nkasi Sh. milioni 16 kutokana na halmashauri hizo kuwa na malimbikizo ya wadaiwa kodi ya pango la ardhi.

Habari Kubwa