Malecela ataka machifu wamsaidie Rais Samia

19Dec 2021
Anjela Mhando
MOSHI
Nipashe Jumapili
Malecela ataka machifu wamsaidie Rais Samia

WAZIRI Mkuu Mstaafu,  John Malecela amewataka Machifu wote nchini kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kuitawala nchi na kuendeleza amani iliyopo kwasababu bila amani hakuna kinachoweza kufanyika.

Malecela  ambaye ni mlezi  wa Umoja wa Machifu Tanzania (UMT), alitoa kauli hiyo jana  alipokuwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa tisa wa UMT uliofanyika katika ukumbi wa Kibo Hotel Marangu  mkoani Kilimanjaro.

Alisema bila amani nchini haiwezi kuwa na maendeleo, bila amani hakuwezi kuwa na kuabudu kwa uhuru. "Kama nyumba haina amani  hiyo inakuwa sio nyumba, nchi kama haina amani sio nchi hivyo ninyi Machifu mkamsaidie Rais (Samia Suluhu Hassan) wetu kuitawala nchi." alisema Malecela na kuongeza kuwa;

"Nianze kwa kuwahikikishia mimi nimekubali kuwa mlezi wa UMT nikiamini kwamba mimi na ninyi Machifu wote mlioko hapa tupo pamoja kuunga mkono serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan."

"Niwajibu wetu sisi wote kutambua na kufanya kila linalowezekana kumsaidia Rais (Samia) ili Serikali ya Awamu ya sita iweze kufaulu, nashukuru na ninyi mmemfanya kuwa Chifu mkubwa wa Machifu wote Tanzania, asanteni sana kwa uamuzi huo  kwasababu na sisi tumemuomba awe Chifu ndio kusema kwamba pia tutachukua nafasi hiyo ya kumtii anapotoa amri halali za kiserikali tutamtii na kumsaidia," alisema

Kwaupande wake Mwenyekiti wa UMT, Frank  Marialle, alisema; "Matumaini yetu kama viongozi wa Machifu wote ni kuisaidia Serikali kama ambavyo machifu wa zamani walivyokuwa wanasaidia katika uongozi  na kurudisha maadili katika jamii zetu zinazotuzunguka;" alisema.

Habari Kubwa