Malinzi ahukumiwa kulipa faini mil.1.5/-

12Dec 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Malinzi ahukumiwa kulipa faini mil.1.5/-

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewahukumu aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na katibu mkuu wake, Selastine Mwesigwa, kulipa faini ya Sh. milioni 1.5 au kwenda jela miaka minne.

Vigogo hao walitiwa hatiani kwa makosa ya kughushi muhtasari wa kubadilisha watiasaini wa akaunti za (TFF kwamba kamati ya utendaji imepitisha mabadiliko hayo.

Pia imemtia hatiani Mwesigwa kwa kosa la nne la kuwasilisha muhtasari wa kughushi benki kwa ajili ya kubadilisha watiasaini.
Washtakiwa hao wanatakiwa kulipa kosa la kwanza Sh. 500,000 kila mmoja au jela miaka miwili.

Katika kosa la pili, Msigwa peke yake alitakiwa kulipa faini ya Sh. 500,000 au jela miaka miwili.

Kadhalika, Mahakama hiyo imewaona mshtakiwa wa tatu, Nsiande Mwanga, aliyekuwa mahabusu tangu Juni 2017 na Flora Rauya aliyekuwa nje kwa dhamana kuwa hawana hatia na imewaachia huru.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Maira Kasonde.

Akisoma hukumu hiyo, Kasonde alisema baada ya kupitia ushahidi wa upande wa Jamhuri, Mahakama imewatia hatiani Malinzi na Mwesigwa kwa makosa hayo.

"Mahakama yangu imewatia hatiani kwa makosa mawili, kosa la tatu linawakabili wote wawili kila mshtakiwa atalipa faini Sh. 500,000 au jela miaka mwili na la nne linamkabili Mwesigwa peke yake, atalipa faini Sh. 500,000 au kwenda jela miaka miwili,"
alisema na kuongeza:

"Katika mashtaka ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha, Mahakama yangu imeona hakuna ushahidi wa Jamhuri uliothibitisha makosa hayo dhidi ya washtakiwa."

Aidha, alisema mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa hao katika makosa 18 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha kati ya mashtaka 20 yaliyokuwa yanawakabili.

Akiichambua hukumu hiyo, hakimu alisema kuhusu hoja za mshtakiwa kuikopesha fedha TFF ni kweli alitoa fedha hizo lakini anaungana na Jamhuri kwamba hakufuata taratibu za shirikisho hilo kuhusu mkopo kutoka kwa mtu binafsi.

Kabla ya hukumu hiyo, Wakili wa Utetezi, Nehemia Nkoko, alidai kuwa washtakiwa ni wakosaji wa mara ya kwanza na kwamba wamekaa mahabusu miaka miwili na nusu.

"Malinzi ana miaka 60 kwa hiyo yuko kundi la wazee ana watoto wanaomtegemea na anasumbuliwa na maradhi ya shinikizo la damu," alidai.

Kwa upande wa Mwesigwa, alidai kuwa anategemewa na mama yake mzazi mwenye miaka 89 na ana watoto wadogo wanaomtegemea na kuiomba Mahakama kuwapunguzia washtakiwa hao adhabu.

Hata hivyo, kwa kuwa hukumu hiyo ilisomwa mpaka saa 11:30 jioni, vigogo hao hawakulipa faini kwa kuwa muda wa kazi ulishapita.

Habari Kubwa