Malumbano hoja mawakili yaweka kiporo hatima dhamana ya Mbowe

07Mar 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Malumbano hoja mawakili yaweka kiporo hatima dhamana ya Mbowe

HATIMA ya kutenguliwa uamuzi wa kuwafutia dhamana au kuendelea kukaa rumande kwa Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko itajulikana leo saa 7:00 mchana.

Hatua hiyo ilifikiwa jana na Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam iliyoketi chini ya Jaji Sam Rumanyika baada ya kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili.

Walalamikaji kupitia mawakili Peter Kibatala na Jeremia Mtobesya kwa nyakati tofauti waliwasilisha hoja za rufani.

Katika hoja ya kwanza ya rufani, walidai kwamba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, chini ya Hakimu Mkazi Mkuu (kwa sasa Jaji), Wilbard Mashauri, Novemba 23, mwaka jana, ilikosea kuwafutia dhamana walalamikaji. 

Kibatala alidai kuwa uamuzi wa kuwafutia dhamana washtakiwa una makosa kwa sababu washtakiwa walikuwapo mahakamani Novemba 12 na 23 na kwamba walipewa nafasi ya kujieleza sababu zilizowafanya kushindwa kufika kwenye kesi yao Novemba Mosi na 8, mwaka jana.

Aidha, alidai kuwa mbali na walalamikaji kujieleza, awali wadhamini wao walifika mahakamani kueleza sababu za kukosa siku ya kesi yao.

"Mtukufu Jaji walalamikaji hawakuwapo mahakamani, lakini taarifa zilitolewa na wadhamini wao. Pia walifika mahakamani wenyewe kwenda kujieleza sababu zao. Mbowe alikwenda nje ya nchi na Matiko alitumwa kuliwakilisha bunge nje ya nchi," alidai na kuongeza:

"Tunaiomba mahakama yako itengue uamuzi wa kuwafutia dhamana walalamikaji kwa sababu Mahakama ya Kisutu ilikosea kuwafutia dhamana yao, warudi nyumbani kuendelea na maisha," alidai Kibatala. 

Akiunga mkono hoja za rufani,  Mtobesya alidai kuwa wadhamini wanaingia mkataba na mahakama na endapo siku mtuhumiwa asipofika, mdhamini anawajibika kutoa maelezo mahakamani kwa nini mtuhumiwa hajafika. 

"Walalamikaji walikwenda mahakamani wenyewe bila hata kukamatwa, tunaomba mahakama itengue uamuzi wa Mahakama ya Kisutu washtakiwa waendelee na dhamana, wapate haki yao ya kikatiba," alidai Mtobesya. 

Akijibu hoja za rufani, Wakili wa Serikali Jacqueline Nyantori, alidai kuwa walalamikaji walipewa dhamana na kufutwa kwa dhamana yao si suala la Jamhuri kuibuka mara moja.

Alidai kuwa Juni 22 na Julai 31, 2018, walalamikaji na washtakiwa wengine walionywa na Mahakama ya Kisutu kutokana na mwenendo wao wa kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yao.

"Mtukufu Jaji kati ya Julai 3, 25, 31 na Agosti 2, 2018, walalamikiwa kwa nyakati hizo tofauti walionywa kwa tabia yao ya kutokufika mahakamani wakasababisha kesi kusimama kuendelea kusikilizwa," alidai.
 
Pia alidai kuwa Novemba Mosi, mwaka jana, upande wa Jamhuri ulishindwa kuvumilia na uliibua hoja ya kuiomba mahakama kutoa hati ya kukamatwa washtakiwa.

Nyantori alidai kuwa Novemba 8 mahakama ilikubali kutoa hati ya kukamatwa na walalamikaji walijisalimisha mahakamani Novemba 12, 2018 siku nne baadaye.

"Mtukufu Jaji dhamana ilifutwa kwa nia nzuri ili kesi iendelee kusikilizwa kwa sababu kulikuwa na ucheleweshaji wa makusudi," alidai wakili huyo wa Jamhuri.

Hata hivyo, alidai kuwa kabla ya dhamana kufutwa wadhamini waliitwa kujieleza na waliiambia mahakama sababu ambazo ilizitathmini ikaona hazina msingi.

Alidai kuwa sababu za wadhamini zilikuwa zinajichanganya na kwamba mahakama ilibaini walalamikaji wamekiuka na kuvunja masharti ya dhamana, hivyo walijiondolea haki yao ya dhamana.

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano ya jaji na wakili wa serikali;-

Jaji: Natamani kujua walalamikaji walikamatwa au walikuwa hawakamatiki? 

Wakili: Mtukufu Jaji zilitolewa taarifa, Mbowe alikuwa nje ya nchi na mshtakiwa wa tano ambaye hapa ni mlalamikiwa wa pili.

Jaji: Dhamana ilifutwa siku hiyo walipofika? 

Wakili: Hapana mtukufu jaji siku hiyo walipewa haki ya kusikilizwa na mahakama ndipo uamuzi ukatolewa.

Jaji Rumanyika alisema, amesikiliza hoja za pande zote mbili na mahakama yake itatoa hukumu leo saa 7:00 mchana.
Wiki iliyopita Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufani ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP)  ya kupinga Mbowe na mwenzake kusikilizwa na Mahakama Kuu.

Mbowe na Matiko kwa pamoja wamekata rufani wakipinga kutenguliwa kwa dhamana yao na Hakimu Mkazi Mkuu, (kwa sasa Jaji wa Mahakama Kuu) Wilbard Mashauri.

Katika maombi yao walalamikaji wanadai kwamba Mahakama ya Kisutu ilikosea kufuta dhamana kwa washtakiwa wakati wao wenyewe walifika mahakamani Novemba 12, 2018 na Novemba 23, 2018, pia walihudhuria mahakamani  siku dhamana yao ilipofutwa.

Novemba 23, 2018, Mahakama ya Kisutu, iliyoketi chini ya Hakimu  Mashauri iliwafutia dhamana Mbowe na Matiko  baada ya kushindwa kufika mahakamani kusikiliza kesi yao ilipopangwa kati ya Novemba Mosi na 8, mwaka huu.

Hakimu alisema Novemba Mosi, mdhamini wa Mbowe alidai mahakamani kwamba ameugua ghafla yuko mahututi hawezi kuongea na amepelekwa kutibiwa nje ya nchi.

Pia wakili wa utetezi, Peter Kibatala, alidai kuwa mshtakiwa ni mgonjwa mahututi amepelekwa nchini Afrika ya Kusini. 

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alipinga sababu zilizotolewa na utetezi na kuiomba mahakama kuuamuru utetezi kuwasilisha vielelezo kuhusu maradhi ya Mbowe.

Mahakama iliamuru washtakiwa wakamatwe na kufikishwa mahakamani kujieleza kwanini wasifutiwe dhamana. Novemba 12, Mbowe na Matiko walijisalimisha mahakamani.

Mbowe wakati akijitetea ili asifutiwe dhamana alidai kuwa aliondoka nchini Oktoba 28, mwaka jana, kwenda Marekani na alianza kuugua akiwa huko Oktoba 31.

Alidai kuwa Novemba 2, alikwenda nchini Ubelgiji wakati akisubiri ahadi ya kuonana na daktari wake Novemba 8 na kwamba alishauriwa asisafiri mwendo mrefu akiwa angani.

Kwa upande wake, Matiko alidai kuwa  alishindwa kufika mahakamani kwa sababu alihudhuria mkutano wa michezo kwa mabunge ya Afrika Mashariki akiiwakirisha Tanzania.

"Kwa kuwa mshtakiwa wa kwanza taarifa zake zinakinzana, hati yake ya kusafiria inatofautiana na maelezo yake, mshtakiwa wa tano pia sababu zake hazina mashiko, mahakama yangu inawafutia dhamana kuanzia leo," alisema Hakimu Mashauri.

Katika kesi ya msingi, mbali na  Mbowe na Matiko, washtakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu;  Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Bunda, Ester Bulaya; na Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Vincent Mashinji.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, mwaka jana jijini Dar es Salaam.

Habari Kubwa