Mama aachiwa huru kesi ya mauaji ya mwanae

13Dec 2018
Joctan Ngelly
KIGOMA
Nipashe
Mama aachiwa huru kesi ya mauaji ya mwanae

MAHAKAMA Kuu Tanzania Kanda ya Tabora, imemwachia huru mkazi wa Kijiji cha Minyinya Wilaya ya Kibondo, Ester Ndalaba (40), baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha kosa la mauaji ya mtoto mwenye umri wa miaka 8.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji wa Mahakama hiyo, Julius Mallaba, alisema mshtakiwa huyo alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la kumuua mtoto wake Magreth Gaudes kwa kumkata shingoni na kitu chenye ncha kali kwa kukusudia.

Upande wa mashtaka ulikuwa ukiongozwa na wakili wa serikali, Antia Julius, ambao ulipeleka mahakamani mashahidi watano na vielelezo viwili.

Jaji alisema upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kosa hilo la mauaji, hivyo mahakama imemwachia huru mshtakiwa kwa sababu jukumu kubwa la kuthibitisha kosa dhidi ya mshtakiwa ni upande wa mashtaka na kama kuna upande wowote ambao haujaridhika na hukumu hiyo wakate rufani katika mahakama ya rufani.

Upande wa utetezi uliongozwa na wakili wa kujitegemea, Iginatus Kagashe.

Jaji Mallaba alisema mtoto huyo alikuwa ni wa mshtakiwa na alikuwa ni mlemavu wa kuongea, kutotembea na mikono na hadi kifo chake alikuwa na umri wa miaka 8 bila ya kuongea wala kutembea.

Alisema siku ya tukio Mei 4, mwaka 2010 ndipo alipofariki dunia kwa kukatwa shingoni na kitu chenye ncha kali.

Alisema mshtakiwa huyo alihusishwa na kitendo hicho cha mauaji kutokana na kifo cha mtoto huyo kuuawa kwenye chumba cha mshtakiwa huyo.

Kwa upande wake wakili Kagashe alipoulizwa na Nipashe kuhusiana na hukumu hiyo, alisema anaishukuru mahakama kwa kutenda haki kwa mteja wake ambaye alikuwa amekaa mahabusu kuanzia Mei mwaka 2010 hadi jana alipoachiwa huru.

Awali akisoma hati ya mashtaka, wakili wa serikali Antia Julius alidai kuwa Mei 4, mwaka 2010 majira ya asubuhi katika Kijiji cha Minyinya Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, mshtakiwa alimuua mtoto wake Magreth Gaudes mwenye umri wa miaka 8 kwa kukusudia, kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Habari Kubwa