Mama adaiwa kuwaua kwa panga watoto 6 na yeye auawa

15Apr 2019
Halima Ikunji
Tabora
Nipashe
Mama adaiwa kuwaua kwa panga watoto 6 na yeye auawa

MAMA mmoja anayedaiwa kuwa mgonjwa wa akili, Nana Maganga (35), amewaua watoto wake sita kwa kuwacharanga mapanga, tukio lililotokea katika kitongoji cha Mwakilezu, Kijiji cha Luzuko, wilayani Nzega, mkoani Tabora na yeye kuuawa wakati akidhibitiwa asiendeleze mauaji hayo.

Tukio hilo limetokea majira ya saa 11 alfajiri Machi 14, mwaka huu, wakati mama huyo alipowaua watoto wake watano wa kuwazaa na mmoja akiwa mtoto wa kaka yake, huku akijeruhi watu wanne.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Kamishna Msaidizi, ACP Emmanuel Nley, amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo ya watu saba.

Kamanda alisema katika tukio hilo, mwenye nyumba ambaye ni shemeji ya mama aliyefanya mauaji, alimkamata na kuanza kupambana naye.

Kamanda Nley alisema Nana alikuwa ni mgonjwa wa akili, hivyo alikwenda kwa mganga wa jadi ambaye ni shemeji yake kwa lengo la kupatiwa matibabu ndipo mkasa huo wa kuwakata mapanga watoto wake ambao alikuwa amelala nao ulipotokea.

Kamanda Nley alisema kuwa waliomdhibiti Nana, walikana kumuua wakidai walimkamata na kumfunga kamba mikononi na kudai kifo chake kimetokana na yeye kunywa sumu, jambo ambalo kamanda Nley amelikanusha.

Alisema Jeshi la Polisi linawashikilia watu watano akiwamo mume wa Nana na mganga wa jadi kwa tuhuma za kumuua mwanamke huyo na kuongeza kuwa upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili kujua chanzo cha mauaji hayo.

Aliwataja watoto waliouawa kuwa ni Pala Massanja (3), Shija Dotto (2), Nyawele Dotto (2), Sida Dotto (5), Kulwa Dotto (4), Dotto Dotto (4) na mama yao Nana.

Aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Kundi Dotto, Nembwa Dotto, Milembe Massanja na Mwashi Massanja.

Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Godfrey Ngupulla, alisema tukio hilo limeibua hisia kali kwa wananchi kwa kuwa ni mara ya kwanza kutokea, hata hivyo, aliwataka wananchi kuwapeleka hospitali wagonjwa wa akili ili kuepusha madhara kama hayo.

Ngupulla alisema mgonjwa huyo huenda alitumia dawa nyingi za mitishamba hadi kusababisha kuchanganyikiwa na kuanza kushambulia watoto na hatimaye kusababisha mauaji hayo.

Mwenyekiti wa kijiji hicho Jilatu Lukwizu alisema mgonjwa huyo alifika nyumbani kwa mganga huyo ambaye ni shemeji yake Massanja Gisengi, majira ya saa mbili usiku, ndipo walipofanya maandalizi ya kulala na watoto wake na saa 11 alfajiri mama huyo alianza kuwashambulia kwa mapanga hadi kuwaua watoto hao.

Habari Kubwa