Mama Maria ampongeza JPM kwa kuinyoosha CCM

09Dec 2018
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Mama Maria ampongeza JPM kwa kuinyoosha CCM

MJANE wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere, amempongeza Rais John Magufuli kwa jitihada anazofanya kukirejesha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwenye mstari.

Taarifa iliyotolewa jana na Idara ya Itikadi na Uenezi ya chama hicho, ilisema Mama Maria alitoa pongezi hizo jana alipokutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mama Maria alimpongeza pia Dk. Bashiru kwa juhudi kubwa ambazo anaendelea kuzifanya za kumsaidia Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Magufuli za kuirejesha CCM kwenye misingi ambayo Baba wa Taifa aliisimamia.

Ilisema alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri ya ujenzi wa zaidi ya vituo vya afya 200 nchini ndani ya kipindi kifupi cha miaka mitatu  ambavyo alisema vitakuwa mkombozi wa upatikanaji wa huduma za afya hasa kwa mama, watoto na wazee.

Taarifa hiyo ilisema katika mkutano huo, Mama Maria alitoa wito kwa CCM kuendelea kuisimamia serikali na kuimarisha lishe bora kwa watoto, watu wazima na umma ili kujenga taifa imara na la watu wenye nguvu ya kuendelea kuchapa kazi sambamba na kaulimbiu ya Rais Magufuli ya Hapa Kazi Tu!

Pia taarifa ilisema Dk. Bashiru alimshukuru Mama Maria kwa kuendelea kuwajali, kuwakumbusha, kuwashauri na kuwaombea kila anapopata nafasi.

Dk. Bashiru, kwa mujibu wa taarifa hiyo,  alimjulisha Mama Maria kwamba Desemba 17 na 18, mwaka huu,  kutafanyika vikao vya uongozi vya taifa, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa na Halmashauri Kuu ya Taifa na serikali zote mbili, ile ya Jamhuri na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zitatoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa Mwaka 2015 – 2020.

Taarifa hiyo ilisema huo ni mwendelezo wa ziara na mazungumzo ya Bashiru na viongozi, makada na wanachama wa CCM ili kupokea ushauri, kubadilishana nao uelewa, mipango, mikakati na taarifa za ujenzi wa chama.