Mama mwenye watoto wenye ulemavu asaidiwa

11Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
SAME
Nipashe
Mama mwenye watoto wenye ulemavu asaidiwa

WANAWAKE wa maeneo mbalimbali katika mikoa ya Kanda ya Kaskazini wamejitolea kumsaidia mama mwenye watoto watano walemavu, mkazi wa Kijiji cha Gwang’ Kata ya Chome wilayani Same, Nighejiwe Joseph.

Wadau akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Same, Rose Sinyamule na Isabela Mwampamba, wakiwa nyumbani kwa Nighenjijwe Amini, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo yalifanyika nyumbani kwa mama huyo kama hatua ya kuhamasisha wadau kumsaidia. PICHA: ASRAJI MVUNGI

Nighejijwe ambaye ni mjane, analea watoto watano wenye ulemavu wa viungo na mtindio wa ubongo.

Juzi, Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule, aliyekuwa ameongozana na wanawake hao kwenda kumfariji mwanamke huyo shujaa wa malezi, baadhi ya wanawake kutoka mikoa ya Arusha na Kilimanjaro wameahidi kuisaidia familia hiyo.

Wakiwa nyumbani kwa mama huyo, Sinyamule alisema ujasiri alioonyesha mama huyo unapaswa kuigwa na wanawake wote nchini, huku akitoa ombi maalumu kwa wasamaria wema kuendelea kujitolea kumsaidia kumudu uwezo wa kuendesha familia hiyo.

Kuhusu mchango wa serikali, Mkuu huyo wa Wilaya, alisema serikali inaendelea kuweka mazingira ya kuziwezesha taasisi zake zinazosaidia jamii kuelekeza nguvu kumsaidia mama huyo.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Upendo Foundation, Isabela Mwampamba, alisema kuwa baada ya kusikia habari za mama huyo na kufika nyumbani kwake kumuona, alianza kujitolea misaada mbalimbali ikiwamo kumlipia mfanyakazi wa kumsaidia masuala ya usafi kwa watoto wake.

Alisema pia amechangisha fedha na kufanikiwa kupata zaidi ya shilingi milioni sita ambazo sasa zimewezesha kufanya ukarabati wa makazi ya nyumba yake, kujenga choo cha kisasa na kuweka uzio wa kuimarisha usalama wa watoto hao.

Akitoa shukrani kwa wadau hao, mama wa watoto ambao ni kati ya watoto wanane alionao, ameeleza kuwa watano walipata ulemavu kwa nyakati tofauti muda mfupi baada ya kuzaliwa.

Wakati akipata mtihani huo, mama huyo ameeleza masikitiko yake kuwa alipata matatizo mengi zaidi, baada ya mume wake kufariki dunia.

Habari Kubwa