Mama wa mapacha wanaokula magodoro afunguka, aomba msaada

20May 2022
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Mama wa mapacha wanaokula magodoro afunguka, aomba msaada

KUNA usemi usemao, ukistaajabu ya Firauni, utaona ya Mussa. Ndivyo unavyoweza kueleza, baada ya mama mwenye watoto wawili mapacha kujitokeza hadharani na kupaza sauti, akiomba msaada wa madaktari bingwa, kujitosa kuwatibu wanawe, wanaokula magodoro badala ya chakula.

Watoto mapacha wanaoishi kwa kula magodoro wakiwa na mama yao, Joyce Mrema, nyumbani kwao, Mtaa wa Kanisani, Kata ya Sokoine One, jijini Arusha. PICHA: CYNTHIA MWILOLEZI

Akizungumza na Nipashe jana jijini Arusha, mama mzazi wa watoto hao, Joyce Mrema, alisema watoto wake walianza kuacha kula vyakula vya kawaida hasa vigumu kama mkate, ugali na wali, walipofikisha umri wa miaka mitatu hadi sasa.

Kwa mujibu wa mama huyo,  watoto hao kwa sasa wanakula magodoro kwa kujificha, huku akieleza kuwa ana hofu huenda tatizo hilo linaweza likawasababishia kuziba kwa utumbo unaoruhusu chakula kufika tumboni.

"Nilishawahi kuwapeleka hospitali ndogo ya Levolosi, nikaambiwa wamekosa madini fulani. Nikashauriwa niende nyumba ya Mungu, Mwanga (mkoani Kilimanjaro) nikachukue dagaa niwachemshe na kumekucha niwape wanywe na kuwachemshia ‘corn flower’ za kijani. Najaribu wapi wanakula magodoro tu," alibainisha.

Alisema magodoro ndani yanaisha hali inayomlazimu kwa sasa kuwafungia nje anapokuwa ametoka au anapofanya shughuli zake nje ili kuwadhibiti.

Pia alisema hata akichemsha maziwa au mayai hawali. “Wanakuangalia tu kama unafanya shughuli, wanaenda chooni kumwaga,” alisema.

"Kuna siku niliwakagua mabegi ya shule nikakuta chakula kimewekwa huko kimekauka nikajua kumbe hawali chakula. Wakipewa  wanaficha hadi kinaweka ukungu, kazi ni kula magodoro na nikiangalia matapishi nakuta vipande vya godoro," alisema.

Alisema hata wanapokwenda shuleni wanaiba vifutio vya walimu vya magodoro wanaleta nyumbani wanakula kwa siri.

"Kuna wakati niliwahi pata kesi kwa jirani yangu mmoja walienda kucheza na wenzao wameingia ndani wakaanza kuchokonoa mito ya makochi na kula godoro. Lakini kwa mama yangu huko Ngulelo hapa Arusha, ambaye ni bibi yao, walikwenda huko kuna wakati nako nikaambiwa wakila wanatapika na walipoangalia waliona vipande vya godoro vingi,” alifafanua.

Alisema kutokana na tatizo hilo kwa sasa hana uwezo wa kuwapeleka hospitali kubwa na kazi yake ni ya kufua nguo za watu kwenye nyumba tofauti tofauti.

"Kazi hii napata kipato kidogo na nilianza mwaka 2013 hawa watoto wakiwa na mwaka mmoja na miezi mitatu baada ya baba yao kunikimbia alipokopa fedha kwa watu," alisema.

Alisema baada ya mume wake kukimbia deni hilo na mkopaji alifungua kesi mahakamani anadai Sh. milioni 33, akishinda kesi atauza nyumba yake na kwamba katika kesi hiyo, anasaidiwa na wanasheria wa haki za binadamu.

Kwa mujibu wa mama huyo, katika suala hilo la mkopo, mume wake hakumshirikisha wakati akikopa Sh. milioni tatu lakini kutokana na kukaa nao kwa muda mrefu, deni limeongezeka mpaka kufikia Sh. milioni 33 ambazo hana.

"Lakini sielewi kwa nini watoto wangu wanakula magodoro, sababu hata nikiwa mjamzito nilikuwa napenda kula machungwa sana, kitu ambacho ni tunda hakina madhara," alisema.

Mrema alisema ameshawapeleka watoto hao kwenye maombi sehemu tofauti tofauti wakaombewa lakini bado wameendelea kula magodoro.

"…Kweli naomba msaada Watanzania wanisaidie niwapeleke hospitali kubwa labda watapata matibabu."

Kwa upande wao watoto hao, walisema wanatamani kuacha kula magodoro na hawapendi kufanya hivyo, lakini wanajikuta wanapata hamu ya kula magodoro kila wakati kuliko chakula chochote.

Walisema walishawahi kuwaza kuacha lakini hawajui kwa nini hawawezi kuacha. Wanaomba Watanzania wawasaidie wakatibiwe, ili waache kula magodoro waishi kama watoto wenzao kwa kula chakula cha kawaida.

Watoto hao walisema licha ya mama yao kuwazuia kula magodoro, kila siku wao wanakula kwa kuwa hawawezi kupitisha siku bila kuyala.

Kwa mtu yoyote aliyeguswa kusaidia watoto hao, wakapate matibabu watumie fedha zao kupitia namba za mama wa watoto hao 0763876313 jina Joyce Mrema.

Habari Kubwa