Mambo haya 12 kumpaisha Samia

28Mar 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe Jumapili
Mambo haya 12 kumpaisha Samia

TANZANIA iko katika enzi mpya ya uongozi. Enzi hiyo ni ya Samia Suluhu Hassan, Rais wa kwanza mwanamke katika ukanda wa Afrika Mashariki, ambaye ameshika kijiti cha uongozi baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17 mwaka huu.

rais Samia Suluhu Hassan.

Rais Samia ambaye kabla ya hapo alikuwa Makamu wa Rais, alishika rasmi uongozi Machi 19 baada ya kula kiapo. Kwa kushika wadhifa huo, Samia ameandika rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania.

Kabla ya hapo, alikuwa na rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais tangu kuasisiwa kwa taifa la Tanzania. Tangu ashike wadhifa huo, kumekuwa na mitazamo tofauti kama anaweza ‘kutosha’ katika ‘viatu’ vya mtangulizi wake, akiwa Rais wa Sita wa Tanzania.

Hiyo yote, kwa sehemu kubwa, inatokana na ukweli kwamba haijawahi kutokea katika historia ya Tanzania. 

Lakini wakati wa mazishi ya kitaifa ya Rais Magufuli yaliyofanyika wiki hii katika Uwaja wa Jamhuri jijini Dodoma,aliwatoa hofu Watanzania alivyoeleza kwa kinagaubaga kwamba anatosha. 

“Kwa wale ambao wana mashaka, ‘mwanamke huyu ataweza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania?’ ninataka niwaambie aliyesimama hapa ni Rais…ninataka nirudie, aliyesimama hapa ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye maumbile yake ni mwanamke,” alisema. 

 MAMBO YA KUMPAISHA 

 

Katika kutekeleza majukumu yake na kuthibitisha kuwa anatosha, yako mambo mengi ambayo yatampaisha na kuonyesha anaweza. Miongoni mwa mambo hayo ni; - 

 

DEMOKRASIA 

 

Katika ngwe ya kwanza ya serikali ya awamu ya tano, ilidaiwa kuwa kulikuwa na kuminywa kwa dekomrasia na uhuru wa kukusanyika, hatua ambayo iliwafanya Watanzania kushindwa kutoa madukuduku yao au kuvijenga vyama vyao. 

Kutokana na hali hiyo, wapinzani wana kiu na matamanio ya kuona kama Rais Samia anaweza kulegeza masharti na kuruhusu wapinzani kukutana na kufanya mikutano.  

BUNGE ‘LIVE’

 

Tangu kuanza kwa serikali ya awamu ya tano, Watanzania walikosa uhondo wa kushuhudia moja kwa moja mijadala ya mikutano ya Bunge na badala yake kilichokuwa kikionyeshwa ni Hotuba ya Bajeti na Maswali na Majibu.

Hivi sasa mjadala uliopo ni je, maonyesho hayo mubashara ya bunge yatarejeshwa ili kuona Mambo haya 12 kumpaisha Samia jadala motomoto ikiendelea katika chombo hicho cha kutunga sheria? 

 

NYONGEZA MISHAHARA

 

Hili ni suala ambao limekuwa likigonga katika vichwa vya wengi kutokana na ukweli kwamba tangu mwaka wa fedha wa 2015/16 mishahara kwa watumishi wa umma haijawahi kupandishwa. Sababu kubwa ambayo serikali ilikuwa ikitoa ni kudhibiti mfumuko wa bei. 

Hata hivyo, wafanyakazi hasa watumishi wa umma, mashirika na taasisi za serikali, wana hamu ya kuona kama ukimya huo wa kutopandishwa mishahara utavunjwa. 

Mei Mosi, mwaka huu, ambayo ni Sikukuu ya Wafanyakazi, itafanyika kwa mara ya kwanza Samia akiwa Rais, hivyo macho na masikio ya Watanzania ni kutaka kusikia kama atavunja ukimya na wafanyakazi kuwa na kicheko. 

 

KIKOKOTOO

 

Mwaka 2018, kuliibuka mjadala mkali nchini kuhusu ukokotoaji wa mafao ya wastaafu baada ya serikali kuja na marekebisho ya sheria yaliyolenga kubadili utaratibu wa wastaafu kupewa asilimia 75 ya mafao yao kisha asilimia 25 inayobaki kupewa kidogo kidogo kila mwezi na kuwa kinyume chake.

Hayati Rais Magufuli aliingilia kati suala hilo na kuagiza kikokotoo kipya kianze kutumika mwaka 2023. 

Kitakachompaisha Rais Samia katika hili ni kuendelea na kikokotoo cha zamani.

 

MIRADI MIKUBWA

 

Katika serikali ya awamu ya tano, kumekuwa na kasi ya utekelezaji wa miradi mikubwa katika sekta za afya, masoko, maji, umeme, reli ya kisasa, ujenzi wa barabara na madaraja ambayo inagharimu mabilioni ya shilingi. Miradi hiyo imeifanya serikali ya awamu ya tano kupata sifa kubwa kwa kuwa imesaidia kutatua matatizo yaliyokuwa yakiwakabili wananchi. Kama Rais samia alivyosema baada ya kula kiapo kuwa “hakitaharibika kitu”, Watanzania wana imani kuwa kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo itakuwa kama mwanzo au zaidi. 

 

RUSHWA NA UFISADI 

Serikali ya awamu ya tano imekuwa ikipambana na vitendo vya rushwa na ufisadi ambavyo kwa muda mrefu vilirudisha nyuma maendeleo ya nchi. 

Katika kutekeleza hilo, serikali ilianzisha Mahakama ya Uhujumu Uchumi, maarufu kama Mahakama ya Mafisadi. 

Watu wengi waliotuhumiwa na kuhusika na vitendo hivyo wamefikishwa mahakamani na wengine kuchukuliwa hatua. 

Ni imani kwamba kasi hiyo itaendelea katika uongozi wa Rais Samia. 

 

ULINZI, USALAMA

 

Vitendo vya ujambazi na ujangili katika hifadhi za taifa vilikithiri kwa muda mrefu. Lakini katika uongozi wa awamu ya tano, vitendo hivyo vimepungua kwa kiasi kikubwa na serikali kupata sifa kemkem. 

Ni imani kwamba hali hiyo ya kuimarishwa kwa ulinzi na usalama itaendelezwa katika uongozi wa Rais Samia na Tanzania kuendelea kuwa shwari kwa maana ya wananchi, mali zao na maliasili za taifa. 

 

ELIMU 

 

Sekta ya elimu imepiga hatua kubwa ndani ya uongozi wa Dk. Magufuli na Rais Samia katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2015. 

Mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na ongezeko la wanafunzi elimu ya awali hadi chuo kikuu, kuongezeka kwa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ni dhahiri kwamba chini ya uongozi wa Samia, sekta hiyo ambayo ni tegemeo la maendeleo ya taifa, itazidi kupewa kipaumbele kama ilivyoainishwa katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kama ambavyo imekuwa ikitekelezwa.  

MAKUSANYO MAPATO

 

Msingi mkuu wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni makusanyo ya maopato ya kodi na yasiyo ya kodi. Ndani ya miaka mitano, kumekuwa na ongezeko la ukusanyaji wa mapato, hivyo kuifanya serikali kupata sifa kutokana na kazi hiyo. 

Mwaka 2015 wakati Dk. Magufuli na Rais Samia wanaingia madarakani, wastani wa makusanyo ya mapato ulikuwa Sh. bilioni 850 kwa mwezi lakini hadi mwaka huu uliongezeka hadi kufikia wastani wa Sh. trilioni 1.4.

Kasi hiyo ya ukusanyaji wa mapato, ni dhahiri kwamba itaongezwa ili kutimiza ndito za kufikia wastani wa Sh. trilioni mbili au zaidi kwa mwezi. 

 

NISHATI

 

Tanzania hivi sasa iko katika mkakati wa kufikia uchumi wa kati ambao unabebwa na dhima ya maendeleo ya viwanda.

 Ili kufikia azma hiyo, suala la nishati hasa umeme wa uhakika ni la muhimu. Katika kutambua hilo, pamoja na mambo mengine, kuna ujenzi wa mradi wa umeme katika Bwawa la Nyerere kwenye Mto Rufiji.

Kukamilika kwa mradi huo, kutawezesha kupatikana kwa megawati 2,115 ambazo zitawezesha Tanzania kuwa na umeme wa ziada ambao utachochea maendeleo ya viwanda na hata ziada kuuzwa nje. 

Kasi hiyo pamoja na utafutaji wa vyanzo vingine vya nishati itaendelea chini ya Rais Samia, hivyo kuleta mapinduzi ya viwanda.

 

VYOMBO VYA HABARI

 

Kilio kikubwa kwa wanahabari kimekuwa kuminywa kwa uhuru wa vyombo vya habari. Kilio hicho kiliambatana pia na madai ya kukosa matangazo kutoka idara na taasisi za serikali, hivyo kulazimu baadhi ya vyombo vya habari kufungwa kutokana na ukata. 

Swali linalotanda katika tasnia hiyo ni, je, hali hiyo itaendelea au italegezwa? Sambamba na mambo hayo, pia Watanzania wana kiu ya kuona kama nidhamu katika utumishi wa umma itaendelezwa katika kasi ile ile pamoja na ujenzi wa masoko katika maeneo mbalimbali ambapo kumekuwa na ujenzi wa miundombinu ya kisasa na wafanyabiashara wananufaika nayo. 

Habari Kubwa