Mambo 10 uchaguzi Konde, Mbagala leo

18Jul 2021
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe Jumapili
Mambo 10 uchaguzi Konde, Mbagala leo

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imevitaka vyama vya siasa, wagombea na wadau wa uchaguzi mdogo unaofanyika leo, kujiepusha na matukio yenye viashiria vya uvunjifu wa amani huku ikitaja mambo 10 ya kuzingatiwa.

Ofisa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Michael Simba (kushoto), akitoa mafunzo kwa wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya vituo, kwa ajili ya kusimamia uchaguzi mdogo wa Ubunge Jimbo la Konde, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba juzi, unaotarajiwa kufanyika leo. PICHA: NEC

Uchaguzi huo mdogo unatarajiwa kufanyika leo katika Jimbo la Konde visiwani Zanzibar na kata mbili za Mbagala Kuu na Mchemo zilizoko Tanzania Bara.

Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji mstaafu Semistocles Kaijage, alitoa angalizo hilo juzi alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi huo.

Aliwataka wapigakura kuondoka vituoni mara baada ya kupiga kura ili kujiepusha na mikusanyiko kwenye vituo hivyo.

Alisema vyama hivyo na wasimamizi wa uchaguzi wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi na iwapo kutakuwa na malalamiko, taratibu za kisheria na kanuni zinapaswa kufuatwa katika kuyashughulikia.

Mwenyekiti huyo alisema uchaguzi utahusisha vyama vya siasa 14 vilivyosimamisha wagombea, wapigakura 66,441 na vituo vya kupigia kura vitakuwa 233.

Alitaja mambo ya kuzingatiwa kuwa ni pamoja na kutojihusisha kufanya mikutano ya kampeni zaidi ya saa 12 jana jioni na haitaruhusiwa kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni.

Mengine ni upigaji kura utafanyika katika vituo vilevile vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, vituo vya kupigia kura kufunguliwa saa moja asubuhi hadi saa 10 jioni.

“Watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu ambao wamo kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwenye jimbo na kata husika na wawe na kadi za mpigakura ambapo kwa Jimbo la Konde ni wale tu walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapigakura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC),”alisema.

Mwenyekiti huyo alisema tume imeruhusu kwa mujibu wa sheria wapigakura waliopoteza kadi zao au kuharibika, kutumia vitambulisho mbadala ikiwamo hati ya kusafiria, leseni ya udereva au kitambulisho cha NIDA.

“Mpigakura aliyepoteza kadi yake au kuharibika ataruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala, iwapo tu atakuwa ameandikishwa kwenye daftari hilo na jina lipo kwenye orodha ya wapigakura katika kituo anachokwenda kupiga kura na majina yake yafanane na yaliyopo kwenye kitambulisho mbadala,” alifafanua.

Kuhusu watu wenye ulemavu, Jaji Kaijage alisema kutakuwa na majalada ya nukta nundu katika vituo vya kupigia kura kwa ajili ya watu hao kupiga kura bila usaidizi na kwa watakaoshindwa kutumia, wataruhusiwa kwenda vituoni na watu watakaowachagua wenyewe kuwasaidia kupiga kura.

“Katika vituo vya kupigia kura, kipaumbele kitatolewa kwa wagonjwa, watu wenye ulemavu, wazee, wajawazito na kinamama wanaonyonyesha watakaokuwa na watoto vituoni,” alisema.

Alisisitiza vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo vina wajibu na haki ya kuweka mawakala katika vituo hivyo na kujumlisha kura.

Alitoa wito kwa wapigakura kujitokeza kwa wingi kwenye vituo vya kupigia kura ili kuchagua viongozi wanaowataka.

Habari Kubwa