Mambo 10 yanayomfanya Chalamila RC wa kipekee

10Jan 2021
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe Jumapili
Mambo 10 yanayomfanya Chalamila RC wa kipekee

TAYARI ana miezi 18 au kwa lugha nyepesi mwaka mmoja na nusu, Albert Chalamila amevaa joho la Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Kufika kwake kwenye mkoa huo, ambao pia una hadhi ya makao makuu ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, kuna aina fulani ya upekee katika wasifu wake, zaidi kazini na hata wakati mwingine nje ya mahali hapo.

Jicho la Nipashe mara zote lilipomwangazia akiwa kazini, ana aina fulani ya wasifu; kwanza ni mchangamfu kupitiliza na masihara ndipo mahali pake, lakini ndani ya angalizo ukivuruga, kilichomfanya Rais amteue kwenda kutumika Mbeya, utashuhudia ukali wake 'kisawasawa'.

Ndani ya masihara hayo, hufikia hatua anakosa 'breki' kuanika joto la jiwe lililomkuta nje ya ofisi na anapokuwa kikazi, tangu siku za mwanzo aliibuka na mtindo analiacha gari lake na kuingia mtaani kujumuika na 'washikaji' mbalimbali wakiwamo wadau kwenye vijiwe vya bodaboda.

Hapo wanabadilishana mawazo mawili matatu, lakini ukizama kwenye dozi yake, daima kuna darasa kwa vijana hao wakipewa kwa lugha ya 'kishikaji' na si haba anapowaaga, mkono wake unakuwa umekunja karatasi fulani ambayo pindi anapowaachia, sura yao ya tabasamu hadi jino la mwisho inakuwa bayana.

Staili hiyo ya kuvuka kwa mguu ndiyo alitumia hata kuvamia kirafiki Soko Kuu la Mwanjelwa jijini Mbeya, vivyo hivyo siku nyingine alipofika katika Hospitali ya Rufani ya Kanda jijini na kuzungumza na kirafiki kwa kina na 'wala unga' wanaolelewa katika kituo maalum.

Pia, isisahaulike, siku zake zikiwa zinahesabika tangu aanze kuanza makazi na ofisi jijini Mbeya, aliorodhesha mambo kadhaa ya kimaendeleo, lakini wahalifu aliwaanikia kwamba ni 'paka na panya' ikitilia maanani alishanong'onezwa na mafaili yanamweleza kwamba watu hao wanapatikana kwa wingi mahali hapo.

Chalamila, alivalishwa viatu vya mtangulizi wake, Amos Makalla aliyehamishiwa Mkoa wa Katavi, kupitia uteuzi wa Rais John Magufuli wa Julai 2018, akitokea Iringa, mkoa alikozaliwa, alikokuwa Mwenyekiti wa Mkoa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Chalamila, kiongozi mwenye sura mbili za umaarufu, uamuzi mgumu na mbwembwe na kiutendaji ambazo zina kawaida ya kuwaacha mashuhuda wa matukio yake midomo wazi, ama kwa vicheko au mshangao wa alichokiamua.

 

Yafuatayo ni mambo 10 yaliyofanywa na kiongozi huyo katika wadhifa wa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya:

KAMATA KIJIJI KIZIMA

Agosti 15, 2018, ikiwa ni siku chache baada ya kuanza kazi mkoani Mbeya, Chalamila aliliagiza Jeshi la Polisi kuwakamata na kuwasweka ndani wananchi wote (zaidi ya 500) wa Kijiji cha Ngole kilichoko Kata ya Ilungu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.

Wananchi hao walikuwa wanatuhumiwa kuhujumu miundombinu ya Mradi wa Maji wa Kijiji jirani cha Mashesye kwa kukata mabomba na kubomoa chanzo cha mradi ambao uliogharimu Sh. milioni 27.

Agizo hilo liligeuka gumzo kwenye vyombo mbalimbali vya habari vikiwamo vya ndani na nje ya nchi, huku baadhi ya watetezi wa haki za binadamu wakimtuhumu kukiuka haki za binadamu.

Hata hivyo, agizo hilo lilizaa matunda kwa kuwa siku chache baada ya utekelezaji wake kuanza, wananchi wa kijiji hicho walikiri kufanya makosa na kukubaliana kuchangishana fedha kwa ajili ya kurejesha miundombinu ya mradi huo katika hali yake ya awali, wakasamehewa.

ACHARAZA VIKOBO WANAFUNZI

Oktoba 3, 2019, Chalamila aliwacharaza bakora wanafunzi 14 wa Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya ambao walikuwa wanatuhumiwa kuchoma bweni la shule hiyo kama sehemu ya kulipiza kisasi baada ya kupokwa simu walizokuwa wanamiliki kinyume cha miongozo.

Hakuishia kuwashushia bakora tu. Siku iliyofuata, alirejea tena shuleni huko na kuwatimua wanafunzi wote wa kidato cha tano na sita (walikuwa 392).

Aliwataka wanafunzi hao kurejea shuleni baada ya wiki tatu na kila mmoja kutakiwa kulipa Sh. 200,000 kwa wale ambao hawakukutwa na simu na wale waliokutwa na simu, walitakiwa warejee na Sh. 500,000.

Baada tukio hilo, kuwa na minong'ono kwamba huenda kiongozi huyo angechukuliwa hatua na Rais Magufuli, lakini ikawa kinyume cha matarajio hayo kiongozi huyo wa nchi alipojitokeza hadharani na kumpongeza kwa hatua hiyo.

Baada ya wanafunzi kutekeleza adhabu hiyo, zilikusanywa Sh. milioni 82 ambazo zilitumika kukarabati mabweni hayo mawili na kujenga bweni jipya ambalo lilipewa jina la Chalamila.

SKIMU YA UMWAGILIAJI

Mwaka 2018 uliisha vibaya kwa wakulima takribani 5,000 wa Skimu ya Umwagiliaji ya Mnazi iliyoko Kata ya Imalilo- Songwe wilayani Mbarali baada ya Chalamila kusimamia uvunjaji wa chanzo cha maji na kufukia mfereji wa skimu hiyo.

Shida ni nini? Alichukua uamuzi huo ili kulinda ikolojia ya Mto Ruaha baada ya maofisa wa Bonde la Maji la Mto Rufiji kudai kuwa mfereji huo ulichimbwa na wakulima hao bila kuwa na kibali na ulikuwa miongoni mwa mifereji isiyozingatia matumizi endelevu ya maji.

Siku iliyofuata, alirejea katika kata hiyo na kuwataka wakulima hao wajenge upya mfereji huo kwa maelezo kuwa Rais John Magufuli alimpigia simu na kumwelekeza awasamehe wahudumie mazao hayo kwa msimu huo pekee.

TEMBEZA MKONG'OTO USIKU KUCHA

Agosti 6, 2019, baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Makwale wilayani Kyela, waliushambulia kwa mawe msafara wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo na kuyaharibu baadhi ya magari likiwamo lililokuwa linatumiwa na maofisa wa usalama.

Wananchi hao walifanya tukio hilo kwa madai kuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Cloudia Kitta, alikuwa anawatetea 'wachawi' wa kijiji hicho akiwamo mama aliyetuhumiwa kumuua mtoto wake kwa imani za kishirikina.

Tukio hilo lilimkera Chalamila, akatoa amri kwa Jeshi la Polisi kuweka kambi katika kijiji hicho na kutembeza mkong’oto kwa wananchi hao usiku kucha ili liwe fundisho kwa wananchi wengine.

Chalamila pia aliagiza wananchi hao kulipa gharama za matengenezo ya gari iliyoharibiwa.

MSHAHARA UNATOSHA 'MCHEPUKO'

Aprili mwaka jana, Rais Magufuli alizuru mkoani Mbeya kwa mara ya kwanza tangu alipochaguliwa kushika nafasi hiyo katika awamu yake ya kwanza.

Katika mkutano wake uliofanyika kwenye Uwanja wa CCM Ruanda Nzovwe, Chalamila alikuwa miongoni mwa wazungumzaji na alipopata fursa hiyo, alitamka maneno ambayo yalichekesha wengi.

"Mheshimiwa Rais, ninashukuru unanilipa mshahara mzuri ambao unanitosha hata kukaa na 'kamchepuko kidogo', wachungaji mnisamehe, nilikuwa ninachomekea tu," alisema Chalamila.

Maneno hayo yalionekana kutomfurahisha Rais Magufuli, japo siku hiyo hakuzungumzia chochote hadi Aprili 27 alipoendelea na ziara yake wilayani Chunya ambako pia Chalamila alitamka maneno yanayofanana na hayo.

"Mheshimiwa Rais, ninashukuru umeniletea DC (Mkuu wa Wilaya) mzuri,” alisema Chalamila akimlenga Maryprisca Mahundi, sasa Naibu Waziri wa Maji.

Maneno hayo yalionyesha kumkera Rais Magufuli ambaye katika hotuba yake siku hiyo alisema amesikitishwa kutokuanzishwa kwa soko la madini wilayani huko licha ya kutoa agizo muda mrefu huku Mkuu wa Mkoa akionyesha kupenda 'michepuko'.

KUFUFUA WAFU

Mwaka 2019, Mkoa wa Mbeya ulikuwa miongoni mwa mikoa iliyokuwa na waganga wa jadi wengi waliotuhumiwa kupiga ramli chonganishi na kuchochea migogoro kwenye jamii, huku wananchi wakitaka serikali iruhusu shughuli hizo kuendelea.

Chalamila akiwahutubia wananchi wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mbalizi, alisema kama waganga hao wanataka awaruhusu kufanya kazi hiyo, wanatakiwa waende katika Chumba cha Kuhifadhia Maiti cha Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Mbeya na kufufua maiti ili waaminiwe.

Alisema kama hawawezi kufanya hivyo, hawezi kuruhusu kazi yao iendelee na akaagiza vyombo vya dola kuwashughulikia endapo watakamatwa wakifanya kazi hiyo...soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa