Mambo 6 tozo miamala ya simu

19Jul 2021
Na Waandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
Mambo 6 tozo miamala ya simu

SIKU chache baada ya utekelezaji wa bajeti ya serikali ya 2021/2022 kuanza na wananchi kulalamikia tozo za miamala ya simu, mambo sita yametajwa yatakayoleta mapinduzi katika tozo hizo.

Tozo hizo zimefafanuliwa kuleta faida kwenye uboreshaji wa barabara za vijijini, kuboresha shule za vijijini, hospitali za vijijini na kupeleka vifaa tiba.

Pia tozo hizo zimeelezwa kuwa zitaboresha mifumo ya maji vijijini, mifuko ya jimbo kuwezeshwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na kuboresha Mfuko wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA).

“Kwa mtu yeyote anayejua namna gani ya kukataa utegemezi katika kujenga nchi anakatwa anaumia, lakini anakuwa na tumaini kuwa kesho kinamama wajawazito hawatakufa njiani sababu ya barabara mbovu, wanafunzi watawahi shuleni, wafanyakazi watawahi maofisi na bidhaa za wakulima zitawahishwa minadani na katika viwanda.”

Jana Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, alisema ni lazima Watanzania sasa wafunge mkanda kwa ajili ya kutekeleza bajeti hiyo serikali kwa kuwa imekusudia kuongeza uwezo wa ndani wa kujitegemea kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika maeneo ya vijijini ambako ndiko kwenye uchumi mkubwa na idadi kubwa ya wananchi.

Profesa Kabudi, alisema hayo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Wizara hiyo ya Katiba na Sheria uliofanyika mjini Morogoro na kuambatana na kutembelea miradi mikubwa ya serikali ambayo ni ujenzi wa Reli ya Kisasa (Standard Gauge Rail) na Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere.

Alisema kuwa bajeti ya serikali imelenga kumkomboa mwananchi wa kijijini ili kuhakikisha anaweza kupata huduma bora kama kuwapo kwa miundombinu bora ya barabara ili kuweza kuhakikisha mazao yanazalishwa yanasafirishwa ili kwenda kuuzwa ndani na nje ya nchi ambako ndiko kwenye masoko ya uhakika.

Profesa Kabudi, alisema pia bajeti hiyo imelenga kuhakikisha kunakuwapo na huduma za umeme maeneo yote ya vijijini, ujenzi shule za uhakika pamoja huduma za afya na kwamba ili kuweza kufikia hayo ni lazima serikali ijenge uwezo wa kukusanya fedha za ndani katika vyanzo mbalimbali kutekeleza na sio kusubiri kusaidiwa au kupewa mkopo.

“Nchi yoyote ile ambayo inalenga kuleta mabadiliko ndani ya nchi yake ni lazima inatengeneza mazingira ya kuongeza kukusanya kupitia mapato yake ya ndani, sasa sisi tumeamua kuleta mabadiliko maeneo ya vijiji lazima tuongeze ukusanyaji wa mapato ya ndani na sio kusubiri kupewa mkopo au msaada,” alisema Profesa Kabudi.

Akizungumzia kuhusu miradi mikubwa miwili ya ujenzi wa Bwawa la kufua Umeme la Julius Nyerere na Mradi wa Reli ya Kisasa, alisema serikali ilifanya uamuzi mzuri na wenye faida kwa taifa kwa kuwa utasaidia kuwapo kwa umeme wa uhakika na utachochea kuongezeka kwa viwanda pamoja na reli itakayosaidia kusafirisha mizigo mingi mpaka nchi za jirani.

“Nichukue fursa hii kuwapongeza kwa kutembelea miradi hiyo miwili mikubwa ya kitaifa, nawasihi mkawe mashahidi na mabalozi wazuri juu yanayoendelea katika miradi hiyo huku mkiendelea kuinga mkono serikali ya awamu ya sita katika utekelezaji wake pamoja na mengine yote yanayoendelea ambayo mnayaona,” alisema Waziri Profesa Kabudi.

Awali, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Profesa Sifuni Mchome, pamoja na kikao cha baraza hilo kujadili bajeti ya wizara hiyo, alisema wameona kutembelea miradi hiyo mikubwa miwili kwa kuwa wizara hiyo inahusika moja kwa moja katika sehemu ya utekelezaji wake.

Profesa Mchome, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Baraza hilo, alisema baraza hilo la wafanyakazi ni utekelezaji wa agizo namba moja la mwaka 1970 ukiwa na dhamira ya dhati ya kuwashirikisha watumishi kwenye mipango ya wizara kwa kuwa kila mtumishi anashiriki kwa uhuru na majadiliano ya ajenda zilizoainishwa.

*Imeandaliwa na Ashton Balaigwa, Morogoro na Mwandishi Wetu, Dodoma

Habari Kubwa