Mameneja walivyokufa ajali ya treni

24Mar 2020
Enock Charles
Pwani
Nipashe
Mameneja walivyokufa ajali ya treni

WATUMISHI watano wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), wamefariki dunia katika ajali iliyotokana na treni ya uokoaji kugongana na kiberenge katika eneo lililopo kati ya stesheni ya Mwakinyumbi na Gendagenda katika reli inayotoka Ruvu mpaka Mruanzi mkoani Pwani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano wa TRC, Jamila Mbarouk, tukio hilo lilitokea Machi 22, mwaka huu.

Aliwataja waliofariki ni Meneja Usafirishaji Kanda ya Tanga, Ramadhani Gumbo, meneja ukarabati wa mabehewa ya abiria Kanda ya Dar es Salaam, Fabiola Moshi, Meneja Msaidizi usafirishaji Kanda ya Dar es Salaam, Joseph, Mtaalamu wa usalama wa reli, Philibert Kajuna na dereva wa kiberenge, George Urio.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kati ya watumishi waliofariki, wanne walifariki katika eneo la ajali huku majeruhi wawili wakifikishwa katika Hospitali ya Wilaya ya Magunga iliyopo Korogwe mkoani Tanga kwa ajili ya huduma za kitabibu.

Taarifa hiyo iliongeza kuwa saa tano usiku wa Machi 22 majeruhi mmoja alifariki na kufikia jumla ya watumishi watano.

Aidha, taarifa hiyo ilieleza kuwapo kwa majeruhi mmoja aliyetajwa kwa jina la Elizabeth Bona, ambaye ni mwongoza treni ambaye anaendelea na matibabu.

Alisema uchunguzi kuhusiana na ajali hiyo utafanywa ili kubaini chanzo cha ajali hiyo kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali, ikiwamo Polisi.

Habari Kubwa