Mamlaka zavalia njuga upotevu maji

15Sep 2021
Frank Kaundula
Morogoro
Nipashe
Mamlaka zavalia njuga upotevu maji

MAMLAKA za Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro, Dodoma na Singida zimeanzisha kampeni ya kutokomeza upotevu wa maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo bila matatizo na kwa bei nafuu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA), Mhandisi Tamimu Katakweba, alisema kuwa kitendo cha kupambana na upotevu wa maji ni hazina kwa taifa.

“Kumekuwa na upotevu wa maji unaofanyika kwa njia mbalimbali ikiwamo wizi wa maji na mvujo, hivyo kusababisha mamlaka za maji kupata hasara. Tumeamua  kukabiliana na tatizo hili,” alisema.

Katakweba alisema kitendo cha mvujo wa maji husababisha baadhi ya watu kutopata huduma ya maji ya uhakika lakini pia yanapokuwa yakipatikana huwa na gharama kubwa kitendo ambacho kimekuwa kikisababisa kero kwa wananchi.

Alisema serikali kupitia Wizara ya Maji imeziagiza mamlaka za maji kuhakikisha kero zote za maji zinatatuliwa ili wananchi waondokane nazo jambo litakalosaidia   kuwatua wanawake ndoo za maji kichwani.

Mhandisi Katakweba pia aliwataka wananchi wote kuwa walinzi dhidi ya wanaohujumu miundombinu ya maji kwa kutoa taarifa kwa mamlaka za maji ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kwa wote wakaobainika kuhusika na hilo.

Katakweba aliwataka watumishi wa mamlaka za maji katika mikoa hiyo kuwa wazalendo kwa taifa lao na kuepuka kuwabambikia wateja bili za maji, kuepuka rushwa pamoja na kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa yote hatari.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Sindiga, James Malima, alisema utopevu wa maji ni adui mkubwa kwa mamlaka hizo, hivyo wameamua kukabiliana na tatizo hilo.

Malima aliwataka wasoma mita wote wa mamlaka hizo za Morogoro, Dodoma na Singida kuacha tabia ya kuwabambikia bili wateja kwa kuwa kitendo hicho hakileti picha nzuri kwa mamlaka.

Alex Mpagama, Meneja Biashara wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) alishukuru ushirikiano wa Wizara ya Maji na kusema kampeni hiyo itasaidia kupunguza tatizo la upotevu wa maji.

Habari Kubwa