Manyanya atangaza fursa soko la samaki

23May 2020
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
Manyanya atangaza fursa soko la samaki

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, ametangaza fursa za soko la samaki Kanda ya Ziwa wakati wa mapokezi ya ndege ya Ethiopia Airlines iliyoanza safari zake kuja Tanzania katika mkoa wa Mwanza kuchukua minofu ya samaki ambayo inauzwa katika nchi mbalimbali duniani.

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya, picha mtandao

Manyanya amesema: "Mpaka kufikia Machi, 2020 samaki tani 392,933 wamevunwa nchini na mauzo yameongezeka kulinganisha na miaka miwili iliyopita na mauzo yalikuwa Sh. bilioni 379 na kufikia bilioni 691.88 kwa mwaka 2018/2019. Tani 32,388.88 zenye thamani ya Sh. bilioni 436.97 ziliuzwa nje ya nchi na mapato kwa serikali yalikuwa bilioni 19.1"

Baada ya kushuhudia ndege hiyo ikipakia samaki amewatangazia na kuwadhihirishia wawekezaji wote nchini kuwa kuna soko la samaki la uhakika kwasababu kwa sasa samaki wanafuatwa moja kwa moja mkoani Mwanza na kupelekwa katika maeneo mbalimbali duniani.

“Tanzania tumejaliwa, tunao samaki wazuri na wakutosha na sio Ziwa Victoria pekee tuna maziwa mengine makubwa na Bahari ya Hindi, kwa hiyo naomba niwadhihirishie wawekezaji wote kuwa sasa tuna soko la uhakika la samaki, jitokezeni kuwekeza kwasababu minofu yetu ya samaki inafuatwa moja kwa moja na ndege hadi Mkoa wa Mwanza.”

Vile vile, alisisitiza ndege ya Ethiopia iliyoanza kuingia nchini juzi imepakia kilogramu 17,262 zenye thamani ya Sh. 191,874,837.78 na mrabaha uliolipwa ni Sh. 9,541,301.21 na samaki watauzwa katika nchi za Belgium, Uholanzi, Ujerumani, Ufaransa, Ureno na Australia na kwa upande wa mabondo (fish maws) soko kubwa ni China.

Naye Naibu wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi, Atashasta Nditiye, alisema kuwa safari za ndege ya Ethiopia kuja kuchukua samaki Mwanza ni fursa kubwa kwa wana Mwanza na Kanda ya Ziwa kwa ujumla kwa kuwa kabla ya hapo ilikuwa inakuja ndege ya Rwanda Air mara moja kwa wiki kila Jumanne.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amesema viwanda vitatu vimesafirisha samaki juzi na kuvitaja kuwa Kiwanda cha Victoria Perch limited ambao wamesafirisha tani 5.4 (5,400kg) zenye thamani ya Dola za Marekani 21,600) Kiwanda cha Nile Perch Limited ambacho wamesafirisha tani 8.9 (8990kg), zenye thamani ya Dola za Marekani 35,900 na Kiwanda cha Omega Fish limited kinachosafirisha tani tano (5,000kg) zenye thamani ya Dola 22,320.

Mongella alisisitiza kuwa uzalishaji wa Kanda ya Ziwa kwa wastani kila wiki katika kipindi cha mavuno ni tani 1,100 na kipindi mavuno haba ni tani 220.

Habari Kubwa