Maofisa wawili Nida watumbuliwa

11Jan 2020
Na Mwandishi Wetu
Songea
Nipashe
Maofisa wawili Nida watumbuliwa

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amemwondoa madarakani Ofisa wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) Mkoa wa Ruvuma, Seif Mgonja, kwa madai ya kutogawa kwa wananchi namba za vitambulisho vya Taifa (NID).

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, picha mtandao

Ofisa huyo anadaiwa kutogawa namba hizo kwa wananchi 14,493 tangu Desemba 31, mwaka jana licha ya kuzalishwa na makao makuu ya mamlaka hiyo na kupelekewa ofisini kwake mjini Songea.

Waziri Lugola pia amemwondoa madarakani Ofisa wa Nida Wilaya ya Namtumbo mkoani humo, Thobias Nangalaba, kwa madai ya uzembe kwa kutofika katika kikao chake na viongozi wa mkoa na wilaya, licha ya kupewa taarifa ya kuhudhuria kikao hicho.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Soko Kuu la Manispaa ya Songea jana, Waziri Lugola, alisema, ametengua vyeo vya maofisa wawili hao akidai wamecheza na kazi za serikali, kwa kutojali majukumu yao.

“Ndugu wananchi wa Songea, maofisa hawa wamekuwa wakienda kinyume cha maagizo ya serikali ya kuwataka wawakamilishie wananchi usajili wa laini za simu kwa alama za vidole kwa wakati.

Hivyo, hawatufai na wanapaswa watupishe ili wengine waweze kuiongoza Nida mkoani hapa. Haiwezekani ofisa wa Nida mkoa anacheza na wananchi kwa kutopeleka taarifa ili kupata fursa ya kusajili laini zao ambapo zoezi hilo linatarajia kukamilika Januari 20 mwaka huu," alisema.

Lugola alisema serikali inawajali wanyonge, hivyo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Ndani ya Nchi, anapambana na watu wanaokwamisha jitihada za serikali.

Waziri huyo pia aliitaka Idara ya Uhamiaji mkoani Ruvuma kufanya kazi usiku na mchana wakishirikiana na Jeshi la Polisi kuwasaka wahamiaji haramu, hasa katika eneo la mpaka wa Tanzania na Msumbiji mkoani humo.

“Ndugu wananchi, toeni taarifa za wahamiaji haramu, itasaidia kuwakamata na pia kuwashughulikia ipasavyo kwa kuwa watu hao ni hatari kwa uhalifu," aliiomba.

Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi lipo imara na linaendelea kulinda usalama wa nchi, akidai matukio ya uhalifu mkubwa yamesambaratishwa, na matukio yaliyobaki ni madogo ambayo hayana nguvu katika amani ya nchi.

“Serikali ya Dk. John Pombe Magufuli ipo imara, uhalifu sasa haupo, ujambazi tumeusambaratisha kabisa, kama kuna uhalifu, basi mdogo mdogo tu, huyu kanitukana hivi na vile, lakini matukio ya uhalifu makubwa hayapo nchini, nyie mashahidi na mnaona," alitamba.

Waziri Lugola anaendelea na ziara yake katika mikoa ya kusini na baada ya kumaliza Mkoa wa Ruvuma, anatarajiwa kwenda Mtwara na Lindi.

Habari Kubwa