Maono ya mbali, sera vinavyompaisha Jpm kinyang’anyiro uchaguzi urais

06Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Maono ya mbali, sera vinavyompaisha Jpm kinyang’anyiro uchaguzi urais

KAMPENI za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani zimeanza kwa kasi huku wagombea wakichuana kwa hoja, ubunifu na uwezo wa kushawishi wapigakura na vyama vya siasa na wagombea kunadi ilani na sera zao wachaguliwe ifikapo Oktoba 28, mwaka huu.

Lakini pia kipindi hiki ni mahususi kwa wapigakura kutumia sanduku la kura kuwazawadia wanasiasa waliofanya vizuri na kuwaadhibu walioshindwa kutekeleza ahadi zao kutokana na kuchaguliwa kwao.

Kampeni za mwaka huu zimeanza kwa mbwembwe nyingi zilizoambatana na kaulimbiu kama Tutaleta ubwabwa kuku’ (CHAUMA) na Kazi na Bata (ACT- Wazalendo), Uhuru, Haki na Maendeleo (CHADEMA).

Lakini mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli, kwa ujasiri mkubwa, ameibuka na kaulimbiu inayosomeka; ‘Tumetekeleza kwa Kishindo, Tunasonga Mbele Pamoja’.

Kampeni za uchaguzi huu si kwamba zinafanyika katika muktadha mpya, bali ni mwendelezo wa kilichoanza mwaka 2015.

Kipindi kama hiki miaka mitano iliyopita, CCM, vyama vya upinzani chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na Anna Mghwira (sasa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro) akipeperusha bendera Chama cha ACT Wazalendo, walipambana vikali katika majukwaa ya kisiasa kunadi sera ya mabadiliko.

Miaka mitano imepita kwa kasi ya mwanga na sasa vyama vimekuja tena kufanyiwa tathmini na wapigakura. Katika wiki ya kwanza ya ufunguzi wa kampeni, vyama vikuu karibu vyote, vimezindua ilani zao na kunadi sera zao kwa umma.

Kitu ambacho wapinzani wa CCM wanashindwa kukiri kwa uwazi ni kuwa haikutarajiwa kama Tanzania ingeendesha uchaguzi katika mazingira huru kama ilivyo sasa kutokana na tishio la janga la corona lililolikumba taifa na dunia miezi kadhaa iliyopita.

Wapinzani walishawahi hata kususia vikao vya Bunge wakiituhumu serikali kutolichukulia hatua stahiki janga hili. Katika tweet yake ya Mei Mosi, mwaka huu, mgombea urais wa CHADEMA, Tundu Lissu aliandika kuwa: “Mheshimiwa Rais Magufuli. Utake usitake,

Urais wako wa miaka mitano utaamuliwa na coronavirus na kauli na matendo yako kwenye janga hili! Kwa hiyo tumia wakati huu ukiwa mafichoni Chato kuandaa majibu juu ya ‘kaugonjwa kadogo’ haka na juu ya vifo hivi vinavyoendelea kuongezeka”. Huenda ndugu Tundu Lissu ameisahau tweet hii.

Ni hakika kwamba hakuwa pekee yake katika hofu hii bali kuna Watanzania wengi walikuwa katika taharuki kubwa. Lakini katika hali hiyo tete, Rais Magufuli alionyesha ukomavu wa kiuongozi, maono ya mbali, ujasiri na uthabiti wa kiuamuzi, kuwaelekeza wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kujenga uchumi wa nchi na kipato binafsi; kushinda hofu ya ugonjwa wa corona na kuhimiza maombi maalum kwa Mwenyezi Mungu.

Si kwamba corona imeisha, lakini sasa, wanasiasa hawa hawa wanashindana kuonyesha uwezo wa kuvutia umati kwenye mikutano yao ya kampeni badala ya kuzingatia ‘social distance’ kama moja ya mbinu zilizoelekezwa kujikinga na corona.

Maono hayo yanampa Rais Magufuli alama ya vema juu ya maono ya mbali na uthabiti wa kiuongozi alivyoshughulikia suala hilo mpaka sasa na taifa liko huru kuendesha kampeni zenye mikusanyiko mikubwa.

Kwa muktadha wa sera, kaulimbiu ya Ubwabwa Kuku ya Hashim Rungwe wa CHAUMA ni kinyume cha sheria, kwani zinarudisha vitendo vya takrima ambavyo ni rushwa ya uchaguzi zilizofutwa katika hukumu ya kesi maarufu ya Takrima ya Mwaka 2005.

Katika suala la maakuli, Rais Magufuli anajigamba katika Ilani ya CCM kuwa kuongeza uzalishaji wa chakula kutoka tani milioni 15.5 msimu wa mwaka 2015/16 mpaka milioni 16.9 mwaka 2018/19 wakati mahitaji halisi ya nchi ni tani milioni 14.

Wagombea wote wa ACT- Wazalendo na CHADEMA wamezungumzia kuhusu uvunaji wa rasilimali za taifa, yaani madini na gesi.

Lissu alidhihaki jitahada za seriakli ya Rais Magufuli kushughulikia sekta ya madini, akihoji kuhusu ankara ya kodi ambayo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliwaandikia Accacia katika sakata la makinikia ambapo thamani yake ingeweza kumpatia kila Mtanzania gari aina ya Noah.

Rais Magufuli amefanya kazi kubwa kuweka ulinzi imara katika sekta hii ili iwanufaishe wananchi ikiwamo kufanya marekebisho ya Sheria ya Madini Sura ya 123 ili kuanzisha Tume ya Madini kwa lengo la kuleta ufanisi wa usimamizi wa sekta, kudhibiti utoroshwaji wa madini ghafi nje ya nchi na kuanzisha masoko ya madini.

Pamoja na kuongezeka kwa mapato kutoka mchango wa asilimia 3.4 mwaka 2015 mpaka 5.2 kwa pato la taifa, sekta hii imewapa fursa kubwa wachimbaji wadogo kunufaika.

Kwa upande wa gesi, Bernard Membe na Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, wanamtuhumu Rais Magufuli kushindwa kutekeleza ahadi yake ya kuzifanya Lindi na Mtwara kuwa kitovu cha uchumi wa gesi.

Mradi unaozungumziwa ni wa dola za Kimarekani bilioni 30 (zaidi ya Sh. trilioni 60 za Tanzania), ambazo ni bajeti ya nchi kwa miaka miwili.

Tathmini inaonyesha kuwa, katika muktadha wa giliba na udanganyifu wa miradi ya rasilimali za nchi huko nyuma, ilikuwa busara ya hali ya juu kwa Rais Magufuli kusubiri na kutekeleza mradi katika muda muafaka kwa masilahi ya taifa.

Mwalimu Julius Nyerere, mwasisi wa taifa la Tanzania, aliwahi kunukuliwa akitahadharisha kuwa rasilimali hizi haziozi, kwa hiyo hakuna sababu za kuharakisha kuingia mikataba isiyo na manufaa kwa taifa.

Nchini Msumbiji ambako miradi kama hii inatekelezwa, uzoefu unaonyesha kuwa tayari kuna migogoro inayoibua maswali ya kifisadi na hisia kuwa miradi husika haiwanufaishi wananchi. Zitto na Lissu, ambao wana historia ya kizalendo kupambania rasilimali za nchi,

wanawachanganya wananchi wanapotaka mabeberu wapewe na kuvuna rasilimali hizi, badala ya kushukuru utulivu na tahadhari iliyochukuliwa ndipo washauri namna ambavyo rasilimali hizi zitawanufaisha Watanzania.

CHADEMA na ACT Wazalendo pia zimejenga hoja kuwa wakulima wa pamba (Mwanza) na korosho, mbaazi na ufuta (Lindi na Mtwara) hawanufaiki na mazao yao kutokana na biashara hodhi ya vyama vya ushirika.

Wanasiasa hawa wanapigia chapuo soko huria ambalo kimsingi ni soko ‘holela’ kama vile “kangomba” au kwa kule Mbinga katika zao la kahawa wanaita ‘magoma’, ambao ni madalali wenye historia ya kuwanyonya wakulima.

Utafiti uliofanyika unaonyesha kwamba, mfumo wa stakabdhi ghalani na mauzo kupitia vyama vya ushirika, vina tija kubwa katika kumsaidia mkulima kunufaika na jasho lake.

Mfumo wa stakabadhi ghalani tangu uanze kutumika baada ya kupitishwa Sheria ya Bunge Na. 10 ya Mwaka 2005, umewezesha wakulima kupata bei za ushindani sokoni, kuongeza usimamizi na ubora wa mazao, umesisitiza matumizi ya vipimo rasmi, umejenga mfumo imara wa kitaasisi katika kusimamia mazao vikiwamo vyama vya ushirika.

Pia umerahisisha ukusanyaji wa mapato ya serikali ikiwamo kodi, licha ya kuwapo kasoro ya kuchelewesha malipo kwa wakulima wakati fulani.

Hata hivyo, ushirika umewafanya wakulima kuunganisha nguvu na kuepuka hasara na unyonyaji unaofanywa na soko holela.

Huenda kuna changamoto za kuboreshwa katika mfumo huu, ikiwamo kuviwezesha vyama vya ushirika kuwalipa wakulima malipo ya awali kwa wakati na kuwa na masoko ya uhakika.

Uchaguzi huu pia unashindanisha kiwango cha matarajio ya wagombea. Katika eneo la maono ya mbali ya kiuchumi, Rais Magufuli amewazidi washindani wake kwa kuleta uwiano wa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na uwekezaji katika huduma za jamii kitu ambacho hukioni katika ilani za vyama vya upinzani.

Uwekezaji wa miradi mikubwa kama reli, mradi wa kufua umeme wa Nyerere Mto Rufiji, upanuzi wa bandari, ujenzi wa meli na ujenzi wa barabara, ni miradi ya kimkakati yenye athari chanya katika uchumi.

Miradi hii ambayo imeanza, inampa Rais Magufuli nguvu ya kuomba ridhaa ya Watanzania miaka mitano zaidi ili aimalizie.

Kwa umuhimu wa miradi hii ya kimkakati kwa uchumi, ingetosha kabisa Rais Magufuli awaombe Watanzania wafunge mikanda itekelezwe. Lakini bado yeye alileta uwiano akawekeza katika afya, elimu bure, usambazaji umeme vijijini kwa bei nafuu na kulipa madeni ya wafanyakazi.

Maono haya ya kiuchumi, yanawashawishi wapigakura kupigia kura mwendelezo wa sera dhidi ya kuwapa wagombea wengine majaribio.

Mnyukano wa mwingine kiajenda katika mtiririko huu ni ajenda ya uzalendo na utaifa.

Wagombea urais wa ACT Wazalendo na CHADEMA wakikosoa msimamo wa Rais Magufuli kuwa hahudhurii mikutano ya kimataifa, hajajenga mtandao na viongozi wa mataifa makubwa nje ndiyo maana Tanzania haipati misaada kutoka kwa wafadhili.

Maswali ya kizalendo ya kujiuliza Watanzania ni kwa kiwango gani hawa viongozi wameelewa somo la kujitegemea kiuchumi? Je, wanadhani tu kuwa hao wanaoitwa wafadhili, ambao kimsingi ni mabeberu, wanamwaga pesa tu bure bila kujali masilahi yao?

Mwalimu Nyerere pia alishawahi kusema Watanzania wasitegemee kuwa kule nje kuna wajomba ambao watatoa pesa za bure.

Katika agenda hii, Rais Magufuli anaonekana pia kupata vema, kwani ameiheshimisha Tanzania kwa kusimama na kutekeleza miradi mikubwa kama mradi wa umeme wa Mto Rufiji na miradi mingine kwa pesa za ndani.

Kwa wapigakura, hoja ya uzalendo bado ina mashiko zaidi kwamba Tanzania haiwezi kujenga uchumi imara kwa ‘kujikomba’ kwa wafadhili, ambao wanazitolea macho rasilimali za nchi.

Habari Kubwa